Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa kujitolea wana mchango mkubwa katika kukabili COVID-19

Mfanayakazi wa kujitolea wa UNICEF Rasa Pattikasemkul akiwa kazini Khon Kean kaskazinimashariki mwa Thailand.
UNICEF/Nipattra Wilkes
Mfanayakazi wa kujitolea wa UNICEF Rasa Pattikasemkul akiwa kazini Khon Kean kaskazinimashariki mwa Thailand.

Wafanyakazi wa kujitolea wana mchango mkubwa katika kukabili COVID-19

Msaada wa Kibinadamu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya wafanyakazi wa kujitolea, Umoja wa Mataifa umetumia siku hii adhimu kuangazia wafanyakazi wa kujitolea na mchango wao katika kukabiliana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona au COVID-19. 

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres unamulika wafanyakazi hao katika siku hii kwa kutambua kuwa, “duniani kote, wafanyakazi hao wanasaidia makundi yaliyo hatarini zaidi, wanarekebisha taarifa potofu, wanaelimisha watoto, wanatoa huduma muhimu kwa wazee na kusaidia wahudumu wa afya walio mstari wa mbele.” 

Guterres anasema taratibu kadri dunia inavyojaribu kujikwamua kutoka kwenye janga hili, “wafanyakazi wa kujitolea wataendelea kuwa na dhima muhimu kuelekea uchumi usioharibu mazingira, jumuishi na wenye haki.” 

Amekumbusha kuwa bila shaka kujitolea ni uti wa mgongo wa jamii na kwamba mara nyingi wafanyakazi wa kujitolea wanapofanya kazi na Umoja wa Mataifa wanjenga hisia ya umoja. 

“Wanaimarisha utangamano wa kijamii, na wanahitajika kulinda jamii hususan kwa kufikia wale walio kwenye mahitaji zaidi.” 

Katibu Mkuu amesema ni kwa kuzingatia hilo ndio maana “katika siku hii ya leo ya wafanyakazi wa kujitolea, natoa wito kwa serikali zichagize dhana ya kujitolea, zisaidie juhudi za kujitolea na zitambue michango ya wafanyakazi wa kujitolea katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 

Ametamatisha ujumbe wake akisema, “wafanyakazi wa kujitolea wanahitaji shukrani za dhati.” 

Siku ya kimataifa ya kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ilipitishwa kwa azimio namba A/Res/40/212 la  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 17 mwezi Desemba mwaka 1985. 

Tangu wakati huo, serikali, mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia wamekuwa wakiungana na wafanyakazi wa kujitolea duniani kote kusherehekea siku hii.