Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 168 wamepoteza mwaka 1 wa masomo, hilo nalo ni janga - Guterres 

Katibu Mkuu Antonio Guterres akihudhuria kuoneshwa wazi kwa 'Darasa la Janga' katika Makao Makuu ya UN ili kuangazia hitaji la serikali kuweka kipaumbele kufungua shule.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu Antonio Guterres akihudhuria kuoneshwa wazi kwa 'Darasa la Janga' katika Makao Makuu ya UN ili kuangazia hitaji la serikali kuweka kipaumbele kufungua shule.

Watoto milioni 168 wamepoteza mwaka 1 wa masomo, hilo nalo ni janga - Guterres 

Utamaduni na Elimu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hiI leo Machi 2 ametembelea eneo katika moja ya viwanja vya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, ambalo limetumiwa na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, kutoa wito kuhusu dharura ya elimu iliyotokana na COVID-19 na kukuza ufahamu kuhusu uhitaji wa serikali kuzifungua shule. 

Onesho hilo, lililopewa jina 'Darasa la Janga,' ni darasa la mfano linaloundwa na madawati matupu 168, kila dawati likiwakilisha watoto milioni moja wanaoishi katika nchi ambazo shule zimefungwa, huu ukiwa ni ukumbusho mkubwa kuhusu madarasa ambayo yanasalia wazi kote duniani.  

Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na UNICEF, shule kwa ajili ya zaidi watoto milioni 168 ulimwenguni zimefungwa kabisa kwa karibu mwaka mzima kutokana na sheria za COVID-19. Zaidi, karibu watoto milioni 214 ulimwenguni au sawa na mtoto 1 kati ya 7 wamekosa zaidi ya robo tatu ya masomo yao ya ana kwa ana.   

Katibu Mkuu Antonio Guterres akiwa amepita katikati ya madawati hayo ambayo pia yametundikiwa mabegi ya wanafunzi, amesema, "moja ya matokeo mabaya zaidi ya COVID-19, imekuwa mateso mabaya ambayo watoto, familia, wanapata kwa sababu ya watoto ambao hawawezi kuhudhuria shule. Wengi, kwa bahati nzuri, walikuwa na nafasi ya kufanya kwa njia ya mtandao, lakini kwa watu maskini zaidi ambao hawana mtandao wa intaneti, tuna mamilioni ya watu walio nje ya shule. Na hilo ni janga. Janga kwao, janga kwa nchi zao, na janga kwa siku zijazo za wanadamu." 

Uchambuzi wa UNICEF wa ripoti ya kufungwa kwa shule unabainisha kuwa nchi 14 ulimwenguni zimebaki zimefungwa kwa kiwango kikubwa tangu Machi 2020 hadi Februari 2021. Theluthi mbili ya nchi hizo ziko Amerika ya Kusini na Karibea, na kuathiri karibu watoto milioni 98 wa shule. Kati ya nchi 14, Panama imefunga shule kwa siku nyingi zaidi, ikifuatiwa na El Salvador, Bangladesh, na Bolivia.