UNICEF yafarijika kupokea habari za kuachiliwa wanafunzi 27 waliotekwa Kagara, Nigeria.  

27 Februari 2021

Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF Nigeria, Peter Hawkins kupitia taarifa iliyotolewa hii leo katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, amesema amefarijika kupokea habari iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ya kuachiliwa kwa wanafunzi 27 wa Chuo cha Sayansi cha Serikali huko Kagara, ambao walitekwa nyara kutoka shule yao zaidi ya wiki moja iliyopita na kwamba anatarajia kurudi kwao salama katika familia zao. 

Bwana Hawkins amesema, "wakati wanafunzi walioachiliwa huru wanaporudi kwa familia zao, naungana na familia ya mwenzao Benjamin Habila, aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa shambulio la usiku shuleni. Fikra zangu na sala ziko pamoja na familia ya Benjamin, ambao wamepata hasara kubwa.” 

Aidha kiongozi huyo wa UNICEF nchini Nigeria amesema tukio la kushambulia shule huko Kagara, kama vile lile lililotokea katika shule ya sekondari ya wasichana ya serikali Jangebe kwenye jimbo la Zamfara jana Ijumaa na mengine kama hayo yaliyotokea kabla, hayakutakiwa kutokea na kwamba watoto hawapaswi kulengwa katika mashambulizi, hususani katika maeneo ambayo wanategemea kuwa salama, shuleni.   

“Mashambulio kwenye vituo vya elimu ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto. Watoto hawapaswi kamwe kuwa walengwa wa shambulio na bado, mara nyingi sana nchini Nigeriawamekuwa waathirika wa mashambulio kwenye shule zao.” Hawkins amesisitiza kwa masikitiko.  

Taarifa yake hiyo imefafanua kuwa mashambulio kama hayo si tu yanapuuza haki za watoto kupata elimu, pia hufanya watoto kuogopa kwenda shule, wazazi wanaogopa kupeleka watoto shuleni.  

Hawkins ametoa wito akisema, "tunapokaribisha habari za kuachiliwa kwa wanafunzi wa Kagara waliotekwa nyara, naomba serikali kuharakisha hatua juu ya kuachiliwa na kurudishwa salama kwa wanafunzi waliotekwa nyara wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Serikali Jangebe, na watoto wote wa shule waliotekwa nyara ambao bado hawajaachiliwa." 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter