Tumefarijika kuachiwa kwa watoto mateka lakini kama kuna wanaoshikiliwa waachiwe-UNICEF Nigeria.

Mtoto akikimbia kwenye uwanja katika kijiji jimboni Katsina, Kasakzini Magharibi mwa Nigeria.
UNICEF/Christine Nesbitt
Mtoto akikimbia kwenye uwanja katika kijiji jimboni Katsina, Kasakzini Magharibi mwa Nigeria.

Tumefarijika kuachiwa kwa watoto mateka lakini kama kuna wanaoshikiliwa waachiwe-UNICEF Nigeria.

Haki za binadamu

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Nigeria Peter Hawkins amesema amefarijika kusikia watoto waliokuwa wametekwa nchini Nigeria, baadhi yao wameachiwa huru. 

Hili linakuja karibia wiki moja kamili tangu kutokea shambulio baya kwenye Shule ya Sekondari ya wavulana katika eneo la Kankara katika Jimbo la Katsina, shambulio ambalo lilishtua Nigeria.

“Nimefarijika kusikia kwamba karibu watoto 344 wameripotiwa kuachiliwa jana usiku na tunatarajia kurudi kwao salama kwa familia zao. Ikiwa kuna ambao bado wanashikiliwa, tunatoa wito kwa washambuliaji kuwaachilia watoto wote mara moja. watoto ambao bado wanashikiliwa mateka nchini Nigeria pia wanapaswa kuachiliwa.” Amesema Bwana Hawkins. 

Mwakilishi huyo wa UNICEF ameeleza kwamba kwa wiki moja, wazazi walikuwa wameamka usiku, wakilia na wakisubiri kurudi kwa watoto wao.

“Mawazo yangu na mshikamano viko pamoja na watoto hawa, familia zao na jamii ya Kankara ambao wamevumilia jaribu lisilowezekana wiki hii iliyopita.” Amesema.  

Wiki iyopita, Ijumaa, kulitokea shambulizi lililolenga watoto moja kwa moja,  katikati ya usiku, mahali ambapo watoto wanapaswa kujiona wako salama.  

Bwana Hawkins ameeleza kuwa shule zinapaswa kuwa salama. Watoto hawapaswi kuwa walengwa wa mashambulizi. 

"Mashambulio kwenye vituo vya elimu ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto. Tukio hili ni ukumbusho wa kusumbua wa idadi kubwa ya vurugu zinawapata raia kaskazini magharibi mwa Nigeria, wakiwemo watoto.”  Amesistiza.  

Kiongozi huyo amehitimisha akisema ni lazima hatua zifanyike ili kuhakikisha kuwa shule ziko salama na kwamba watoto wote wa Nigeria wanaweza kusoma bila woga.