Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya tabianchi ni onyo kwa sayari- Guterres

Watu wanaoishi katika visiwa vya Comoro kwenye bahari ya Indi wanahitajhi kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
UNDP Comoros/James Stapley
Watu wanaoishi katika visiwa vya Comoro kwenye bahari ya Indi wanahitajhi kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti ya tabianchi ni onyo kwa sayari- Guterres

Tabianchi na mazingira

Mataifa hayajafikia popote katika kiwango kinachotakiwa kukabili ongezeko la joto duniani, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hii leo huku ikisihi serikali kuchukua hatua thabiti zaidi na za kina ili kufikia malengo ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi ya kuhakikisha ongezeko la joto halizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi ifikapo mwishoni mwa karne hii.
 

Ripoti hiyo ya awali ya uchambuzi imetolewa na sekretarieti ya mkataba wa kimataiwa wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC kuhusu viwango vya nchi cha kuchangia kukabili mabadiliko ya tabianchi, NDCs, ripoti ambayo imetolewa kabla ya mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi COP26 utakaofanyika mwezi Novemba huko Glasgow.

Imebainika kuwa hata baadhi ya nchi zikiongeza juhudi, bado kwa ujumla kile kinachotakiwa hakitafikiwa.
“Leo ripoti ya mpito ya UNFCCC inatoa onyo kwa sayari yetu. Inaonesha kuwa serikali bado hazijafikia popote kukaribia kiwango kinachotakiwa cha kuhakikisha ongezeko la joto halizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kwa mujibu wa mkataba wa Paris,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akichangia ripoti hiyo.

Serikali za kitaifa zina jukumu kubwa la kuleta mabadiliko ya kupunguza uchafuzi.
Unsplash/Daniel Moqvist
Serikali za kitaifa zina jukumu kubwa la kuleta mabadiliko ya kupunguza uchafuzi.

2021 ni mwaka wa kujenga au kubomoa

Guterres amesema mwaka huu wa 2021 ni mwaka wa kujenga au kubomoa katika kukabiliana na dharura ya tabianchi.
“Sayansi iko bayana, kudhibiti kiwango cha ongezeko la joto kisizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi, lazima tupunguza hewa chafuzi kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 kutoka viwango vya mwaka 2010.” Amesisitiza Guterres.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa wachafuzi wakuu kuongeza viwango vyao vya kupunguz utoaji wa hewa hizo chafuzi kwa kumulika malengo yao yam waka 2030 kwenye NDCs zao akiangazia janga la COVID-19 akisema mipango ya kujikwamua kutoka katika janga hilo in fursa ya kujenga dunia inayolinda na kuhifadhi mazingira.

“Watoa maamuzi lazima watekeleze ahadi zao. Ahadi za muda mrefu lazima ziendane na vitendo vya kuzindua muongo wa mabadiliko ambao watu na sayari wanahaha kupata,” amesema Katibu Mkuu.

Ripoti yamulika sehemu ndogo tu ya kile kilichopo

Ripoti hiyo ya UNFCCC imejumuisha mawasilisho ya hadi tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2020, ikionesha kuwa wanachama 75 wa mkataba huo wa UNFCCC ndio waliwasilisha vigezo vipya au vilivyoboreshwa vya NDCs na hivyo kuwa ni asilimia 30 tu kiwango cha hewa chafuzi inayotolewa duniani.

Katibu Mtendaji wa UNFCCC amesema kuwa ripoti hiyo ni sehemu kidogo ya hali halisi ya viwango vya nchi kukabili mabadiliko ya tabianchi wakati huu ambapo COVID-19 inaleta changamoto ya wazi kwa nchi nyingi kukamilisha mawasilisho yao ya mwaka 2020.

Amesema ripoti ya pili itatolewa kabla ya COP26, na ametoa wito kwa nchi hususan zile zinazoongozwa kwa hewa chafuzi na ambazo hazijwasilisha ripoti, zifanye hivyo ili taarifa zao zijumuishwe katika ripoti ya mwisho.

“Tunapongeza nchi wanachama ambazo licha ya changamoto za COVID-19 zimetekeleza wajibu wao kwa mujibu wa mkataba wa Paris na kuwasilisha viwango vyao vya kitaifa kabla ya tarehe ya mwisho, lakini naomba waliosalia watekeleze ahadi haraka iwezekanavyo,” amesema Bi. Espinosa akiongeza kuwa, “Iwapo jukumu hili lilikuwa dharura awali, sasa ni muhimu kupita kiasi.”

TAGS: Tabianchi, UNFCCC, Ajenda 2030