Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu zaidi sasa kukabili dharura ya tabianchi- Guterres

23 Februari 2021

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala kuhusu vitisho vya amani na usalama duniani visababishwavyo na janga la tabianchi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la tabianchi ni changamoto ya ushirikiano wa kimataifa katika zama za sasa.

"Tayari janga hilo linaathiri kila eneo la shughuli za kibinadamu, na hivyo utatuzi wake unahitaji uratibu na ushirikiano katika kiwango ambacho hatujawahi kushuhudia awali. Ushiriki wa vyombo vya ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo Baraza hili, unaweza kuwa na dhima muhimu katika kukabili changamoto hii," amesema Guterres katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao na kuongozwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Jonson ambaye nchi yake ndio inashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Februari.

Hali halisi ya udharura wa tabianchi

Guterres amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa janga la tabianchi linakuza maradufu majanga yaliyopo tayari. "Ambako tabianchi inakausha mito, inapunguza mazao, inaharibu miundombinu, inafanya watu wakimbie makwao, hapo inachochea hatari ya ukosefu wa utulivu na mizozo."

Amesema utafiti uliofanywa na taasisi ya amani duniani ya Stockholm umebaini kuwa nchi 8 kati ya 10 zenye operesheni kubwa za ulinzi wa amani zimekumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi,

Athari za janga la tabianchi ni kubwa zaidi ambako utete na mizozo vimedhooficha mbinu za kukabiliana na maisha; ambako watu wanategemea mitaji asili kama misitu na samaki kwa ajili ya kujipatia kipato, na ambako wanawake ambao ndio wanabeba mzigo mkubwa wa dharura ya tabianchi, hawana haki sawa na makundi mengine.

Mnamo Februari 2020, mji wa Dori ukanda wa Sahel nchini Burkina Faso lilikuwa linahifadhi takriban wakimbizi wa ndani 15,000.
© UNHCR/Sylvain Cherkaoui
Mnamo Februari 2020, mji wa Dori ukanda wa Sahel nchini Burkina Faso lilikuwa linahifadhi takriban wakimbizi wa ndani 15,000.

"Nchini Afghanistan, kwa mfano, ambako asilimia 40 ya nguvukazi inajishughulisha na kilimo, kupungua kwa mavuno kunatumbukiza watu kwenye umaskini, ukosefu wa chakula, na kuwaacha hatarini kutumikishwa na vikundi vya kihalifu na vilivyojihami," amesema Guterres.

Bwana Guterres ameenda mbali zaidi kutolea mfano eneo la Afrika Magharibi ba ukanda wa Sahel akisema zaidi ya watu milioni 50 wanategemea ufugaji ili kuishi na mabadiliko ya mwenendo wa malisho yamechangia katika ongezeko la ghasia na mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

Huko Darfur, kiwango kidogo cha mvua na ukame wa mara kwa mara vinaongeza ukosefu wa usalama na ongezeko la mapigano ya kugombea rasilimali. Matokeo yao ni madhara zaidi kwa wanawake na wasichana ambao wanalazimika kutembea muda mrefu kusaka maji, kuni na hivyo kuwaweka hatarini zaidi kukumbwa na ukatili wa kingono na kijinsia.

Watoto wakitembea katika maji ya mafuriko katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.
© WFP/Musa Mahadi
Watoto wakitembea katika maji ya mafuriko katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.

Tufanye nini sasa? Guterres ataja mambo manne

Guterres anataka kulindwa zaidi wale walio maskini zaidi kwa kuwa ndio wanaobeba mzigo wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi na ndipo anataja mambo makuu manne anayosema anaona kuwa muhimu zaidi.

Mosi, "tunahitaji kujikita zaidi katika kuzuia madhara kwa kuchukua hatua thabiti zaidi dhidi ya tabianchi. Lazima tuhakikishe dunia inarejea katika mstari wa kufanikisha malengo ya mkataba wa Paris wa Tabianchi na kuepusha majanga ya tabianchi."

Pili, amesema zinahitajika hatua za haraka kulinda watu, jamii na nchi maskini dhidi ya madhara yanayoongezeka yasababishwayo na mabadiliko ya tabianchi. "tunahitaji kuongeza uwekezaji mkubwa katika mikakati na miradi ya mnepo na kukabiliana na tabianchi. Nchi zote wahisani na benki za maendeleo za kitaifa na kimataifa ziongeze mgao wao wa ufadhili wa miradi hiyo ya mnepo kwa angalau asilimia 50, na fedha hizi zipatikane kwa wale walio mstari wa mbele wakikabiliana na janga la tabianchi. Nchi tajiri zitekeleze ahadi ya kutoa dola bilioni 100 kila mwaka kwa nchi za kusini."

Tatu ni kuzingatia hoja ya usalama ambayo inapatia watu kipaumbele. "Janga la COVID-19 limeonesha jinsi gani vitisho ambavyo si vya kijeshi vinaweza kusababisha madhara kiasi gani duniani. Kuzuia na kushughulikia umaskini, ukosefu wa usalama na ukimbizi kunachangia kuendeleza amani na kupunguza hatari ya mizozo. Kamati ya tuzo ya amani ya Nobel ilitambua hilo mwaka jana kwa kupatia tuzo hiyo shirika la Umoja wa Mataifa mpango wa chakula la duniani, WFP."

Katibu Mkuu ametaja kipaumbele cha nne kuwa ni kuimarisha ubia nje ya mfumo wa Umoja wa Mataifa akisema, lazima tuendeleza na tujenge uthabiti na wadau mbalimbali, ikiwemo hili Baraza, kamisheni za ujenzi wa amani, taasisi za kimataifa za fedha, mashirika ya kikanda, mashirika ya kiraia sekta binafsi, taasisi za kielimu na wengineo."

UN tayari inachukua hatua

Amesema katika Umoja wa Mataifa "tunafanya kazi kuhakikisha mikakati yetu ya usuluhishi na uchambuzi inafanya kazi kwa kutambua athari za tabianchi nchi. Mathalani nchini Sudan Kusini, uhamasishaji kuhusu athari za tabianchi umesaidia operesheni za ulinzi wa amani kusimamia mazungumzo ya makubaliano eneo moja kuhusu usimamizi wa mifugo.

Guterres ameshukuhuru Uingereza ambayo ni Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Februari kwa kuandaa mjadala huo na kuwaambia washiriki kuwa "2021 ni mwaka wa kujenga au kubomoa katika hatua zetu za pamoja za udharura wa tabianchi."

Vijana ndio suluhisho

Katika mkutano huo, Nisreen Elsaim, mwanaharakati kijana kutoka Sudan amezungumzia jinsi athari za tabianchi zinavyosukuma vijana wa Afrika na wenzao kwingineko kukimbia makwao, jambo ambalo amesema linaweza kuchochea machafuko.

"Nikiwa kijana, nina uhakika vijana ndio suluhisho. Tupatieni fursa zaidi, tusikilizeni na tushirikisheni," amesema Nisreen ambaye ni balozi kijana kwenye kundi la ushauri la Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi.

Amekaribisha azimio la Baraza la Usalama la kuanzisha ujumbe mpya wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, UNITAMS ambao umetaja bayana kuwa suala la mabadiliko ya tabianchi na ushiriki wa vijana kuw a vipaumbele vyake.

UNITAMS imechukua nafasi ya UNAMID ambayo imemaliza muda wake tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2020.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter