Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres amelaani machafuko yaliyosababisha vifo kwa waandamanaji Myanmar

Jua likizama kwenye mji wa Yangon nchini Myanmar.
Unsplash/Alexander Schimmeck
Jua likizama kwenye mji wa Yangon nchini Myanmar.

Guterres amelaani machafuko yaliyosababisha vifo kwa waandamanaji Myanmar

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo Jumapili amelaani vikali machafuko yaliyofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji nchini Myanmar.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wakemjini New York Marekani  Bwana Antonio Guterres amesema duru za Habari nchini humo zimesema wauaji wanaendelea kuwasaka waandamanaji na angalau watu wawili akiwemo kijana barubaru wameuawa na wengine takribani 30 walijeruhiwa na polisi Jumamosi wakati wa maandamano dhidi ya vitendo vya jeshi kuchukua madaraka kwa nguvu katika nchi za Kusini Mashariki mwa Asia 

Katika ukurasa wake wa Twitter leo Guterres ameandika “Matumizi ya nguvu kupita kiasi, vitisho na udhalilishaji dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani ni vitendo visivyokubalika. Kila mtu ana haki ya kukusanyika kwa amani.”

Jeshi lilipora madaraka nchini Myanmar Februari Mosi wakati bunge la nchi hiyo likijiandaa kurejea kazini baada ya ushindi wa chama cha National League of Democracy cha Aung San Suu Kyi katika uchaguzi mkuu wa kidemokrasia uliofanyika Novemba 2020.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote nchini Myanmar kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kurejesha utawala wa kiraia.

Mtaalam wa haki za binadamu apinga machafuko 

Naye mtaalam  huru maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya hali ya haki za binadamu nchini Myanmar Tom Andrews amesema amesikitishwa na kutiwa hofu kubwa na kuongezeka kupotea kwa Maisha ya watu nchini humo.

Leo Jumapili amesema utawala wa kijeshi wa Junta nchini Myanmar unakaza uzi wa ukatili wake.

“Kuanzia matumizi ya mipira ya maji hadi risasi za mpira na mabomu ya kutoa machozi vitatumika dhidi ya waandamanaji na sasa wanajeshi wanafyatua waziwazi risasi dhidi wanaoandamana kwa amani. Unyama huu lazima ukome sasa”ameandika mtaalamu huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mtaalam huyom pia amepinga na kulaani vikali ongezeko la vitendo vya Junta vinavyoonekana kuwa ni vita dhidi ya watu wa Myanmar.