Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idhaa ya Kiswahili ya UN yashinda tuzo ya kimataifa ya Kiswahili ya Shaaban Robert

Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imeshinda tuzo ya kimataifa ya Shaaban Robert kwa kukuza msamiati wa lugha hiyo kimataifa.
UNIC/Ahimidiwe Olotu
Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imeshinda tuzo ya kimataifa ya Shaaban Robert kwa kukuza msamiati wa lugha hiyo kimataifa.

Idhaa ya Kiswahili ya UN yashinda tuzo ya kimataifa ya Kiswahili ya Shaaban Robert

Utamaduni na Elimu

Nchini Tanzania hii leo Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, UN NEWS KISWAHILI imeibuka  mshindi wa tuzo ya kimataifa ya kiswahili ya Shaaban Robert katika kategoria ya ukuzaji wa misamiati. Hii ni mara ya kwanza kwa kipengele hicho kutolewa na kwenye tuzo hizo ambapo tumemuuliza Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, mmoja wa waaandaji wa tuzo hizo utaratibu wa ushindanishi.
 

Kiswahili ni bidhaa sasa

Kwa mujibu wa Bwana Sigalla, kwa wakati huu ambao lugha ni bidhaa waliandalia lugha kama chombo cha mawasiliano, lakini kama pia bidhaa duniani. Sasa bidhaa siyo tu inatakiwa ijitangaze bidhaa, bali bidhaa inatakiwa ionekane bila kujitangaza.

"Sasa katika kuangalia hivyo tukaona tuna kila sababu ya kuangalia je ni watu wangapi wanazungumza Kiswahili, na je akiba yao, benki yao ya maneno inatoka wapi, ndipo tukaamua tuwe na kategoria au kipengele cha ukuzaji wa misamiati , tuwashindanishe watu katika kategoria ya ukuzaji wa misamiati," amesema Bwana Sigalla.

Walishindanisha watu katika vyombo vya ndani na kwa maana ya Afrika Mashariki, Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, tukapata chombo kimojawapo .Lakini tulifika mbali zaidi tukavuka hadi mabara mengine.

Neno -Jifunze Kiswahili
UN
Neno -Jifunze Kiswahili

Amesema kando ya wale wa ndani "ambao wana wajibu na dhima kubwa ya ukuzaji wa kiswahili, tuliangalia na wenyewe tukampata mshindi. Lakini tukaangalia katika radio zilizo nje ya mpaka wa Tanzania katika Kategoria hiyo hiyo ya ukuzaji wa misamiati,  hapo ndipo Radio UN aliibuka kidedea.”

Ukuzaji wa msamiati kupitia matangazo ya UN News Kiswahili

Alipoulizwa ni  kipi ambacho kiliwezesha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuibuka kidedea afisa huyo mwandamizi wa BAKITA amesema,  “Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa au UN News kiswahili imekuwa na mchango mkubwa sana wa ukuzaji wa misamiati hii. Katika taarifa zao ukiangalia, katika mitandao ya kijamii katika matangazo yao ya moja kw amoja kuna kipengele chao cha kujadili. Na katika majadiliano hayo hawajikiti tu kwa Tanzania, bali wanajikita zaidi katika nchi mbalimbali ambako kuna magwiji wa Kiswahili. "

Amesema Idhaa hiyo huzungumza na mtu wa Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na kujaribu kuangalia hii misamiati imekaaje." Lakini pia Tanzania huwa wanazungumza nasi nasi tunazungumza nao na wanarusha misamiati hiyo, tumeona jinsi gani benki, data au akiba ya misamiati waliyo nayo katika mchango wa lugha hiyo ambayo Baraza limeona, kwa maana BAKITA na BAKIZA wote kwa pamoja kama kamati kuu tukaona tutoea tuzo hiyo katika kategoria hiyo.”
Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ni moja ya Idhaa 9 za Idara ya Mawasiliano ya UN, DGS. Lugha zingine ni kireno, kiingereza, kiarabu, kifaransa, kihindi, kihispanyola, kirusi na kichina.