Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Cabo Delgado, Msumbiji; Wananchi 1000 wavuka mto Ruvuma na kuingia Tanzania

Wakimbizi wa ndani katika maeneo ya Alto Gingone, Pemba mkoa wa Cabo Delgado, Msumbiji
UN Mozambique/Helvisney Cardoso
Wakimbizi wa ndani katika maeneo ya Alto Gingone, Pemba mkoa wa Cabo Delgado, Msumbiji

Machafuko Cabo Delgado, Msumbiji; Wananchi 1000 wavuka mto Ruvuma na kuingia Tanzania

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP, lina wasiwasi mkubwa kuhusu ghasia zinazoendelea na kudorora kwa usalama kwenye jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji.
 

Katika eneo hilo hivi sasa, zaidi ya watu 300,000 wamekimbia makazi na vijiji vyao wakiacha mazao yao na tegemeo lao hivi sasa ni msaada wa kibinadamu.

Mwakilishi wa WFP nchini Msumbiji, Antonella D’Aprile amesema, “tuna wasiwasi mkubwa juu ya hali duni ya kibinadamu inayojitokeza Cabo Delgado ambako mapigano na ghasia yamesababisha watu kukimbia makazi yao na sasa hawana chakula wala mbinu za kujipatia kipato. Kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama na kuharibika kwa miundombinu kunamaanisha kwamba uwezo wa kufikia wananchi unazidi kuwa mgumu na sasa na janga la COVID-19 hali inazidi kuwa mbaya.”

Takwimmu za hivi karibuni kutoka mfumo wa utoaji maonyo kuhusu njaa, FWESNET, zinaonesha kuwa jamii zitaendelea kukumbwa na janga la ukosefu wa chakula kiwango cha 3, au IPC Phase 3, hadi mapema mwakani.

Taarifa hizo zinazidi kutia hofu kwa kuzingatia kuwa Cabo Delgado tayari ni ya pili kwa viwango vya juu vya utapiamlo uliokithiri ambapo zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakabiliwa na utapiamlo, “changamoto zaidi ya hizo zinaweza kufanya hali ya wanawake na watoto kuwa mbaya zaidi.”

Vurugu zinatokea katika maeneo ambayo tayari yalikuwa na matatizo mengine kama Cabo Delgado ambako tayari kulikuwa kumekumbwa na matatizo ya mafuriko na umaskini
UN Mozambique
Vurugu zinatokea katika maeneo ambayo tayari yalikuwa na matatizo mengine kama Cabo Delgado ambako tayari kulikuwa kumekumbwa na matatizo ya mafuriko na umaskini

Kwa sasa WFP imesema inahitaji dola milioni 4.7 kwa mwezi kusaidia wakimbizi wa ndani kaskazini mwa Msumbiji na kwamba bila msaada huo shirika hilo litalazimika kupunguza mgao wa chakula mapema mwezi Desemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa WFP nchini Msumbiji, maelfu ya wakimbizi wamevuka mto Ruvuma na kuingia nchini Tanzania hali ambayo inatia hofu ya kwamba mzozo unaweza kuingia upande wa pili.

Hali inatia hofu pia zaidi kwa kuwa Cabo Delgado ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa virusi vya Corona au COVID-19, na hivyo raia wa eneo hilo kukimbilia eneo lingine kunaweza kusambaza virusi hivyo.

Cabo Delgado ni ya pili kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa COVID-19, sasa kukimbilia maeneo mengine kunaweza kusambaza zaidi virusi hivyo- WFP

Licha ya changamoto za kiutendaji, WFP kwa ushirikiano na serikali ya Msumbiji, wamepanga kila mwezi kufikisha misaada ya chakula, vocha za fedha na vyakula vya lishe kwa watu 310,000 kwenye majimbo ya Cabo Delgado, Nampula, na Niassa.

Ghasia Cabo Delgado

Tangu mwaka 2017, Cabo Delgado imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami, mashambulizi ambayo mara kwa mara yamesababisha wananchi kukimbia makazi yao na kusaka hifadhi kwenye majimbo mengine ya Nampula na Niassa.

Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu, majeruhi na hata uharibifu wa miundombinu, miundombinu ambayo tayari imesambaratishwa na kimbunga Kenneth mwaka 2019.