Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka kuwa adui wa tembo hadi rafiki na mtetezi- Edwin Kinyanjui 

Tembo yatima aliyeokolewa huko David Sheldrick kituo cha  Wanyamapori Trust nchini Kenya.
UNEP/Natalia Mroz
Tembo yatima aliyeokolewa huko David Sheldrick kituo cha Wanyamapori Trust nchini Kenya.

Kutoka kuwa adui wa tembo hadi rafiki na mtetezi- Edwin Kinyanjui 

Tabianchi na mazingira

Nchini Kenya kampeni ya kulinda wanyamapori nayoongozwa na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP imezidi kupanua wigo wake ambapo hivi sasa hata watu ambao awali walikuwa adui wa wanyamapori, wamegeuka rafiki na walinzi wakuu wa wanyama hao kama njia mojawapo ya kuhifadhi misitu kama ile ya mlima  Kenya, bali pia bayonuai ambayo ni muhimu kwa viumbe vyote.

Katikati ya msitu mnene kwenye miteremko ya mlima Kenya tunakutana na Edwin Kinyanjui, huyu ni askari wa wanyamapori katika Wakfu wa mlima Kenya. 

Edwin anatupatia simulizi yake akisema,  “nilipokuwa mtoto, nilichukia sana tembo. Tembo walivamia mashamba yetu kwenye miteremko ya mlima Kenya kwa hiyo nilikuwa nawafukuza. Shuleni tulifundishwa umuhimu wa wanyamapori na bayonuai, lakini sikuelewa faida zake. “ 

Hata hivyo alipotimiza umri wa miaka 21 alijikuta akifanya utafiti kuhusu tembo, na kuanza kutambua kuhusu hisia zao, wanavyowasiliana na wanavyolea watoto wao. 

Edwin anasema, “nilianza kuguswa, nilianza kuona wanyama waliojeruhiwa, wengine wanawindwa, siku moja niliona tembo mtoto anawindwa, nilifanya kila niwezalo kumuokoa. Kwa saa tatu nililia mfululizo kwa kuwa iliniuma mno, kwa sababu ya binadamu kutega mitego ya wanyamapori kwa faida zao binafsi. Ndipo ikawa lengo langu kuu kukomesha tabia hii.” 

Wakfu ya Mlima Kenya ulimuitwa Edwin kuongoza harakati dhidi ya majangili kwenye mlima huo kwa ushirikiano na askari wanyamapori wa Kenya, ambapo kadri walivyozidi kuingia ndani ya msituni walishuhudia vitendo haramu vya ujangili, ikiwemo uuaji wa wanyama na ukataji wa miti kiholela, vitendo vikifanywa na jamii zinazozunguka mlima Kenya, kwa lengo la kupata fedha. 

Hata hivyo anasema hivi sasa kwa kufanya kazi na jamii wameibuka na mbinu za kuwawezesha kupata kipato bila kuharibu bayonuai ya mlima Kenya na anaamini kuwa kwa ushirikiano na jamii hiyo wataweza kulinda mlima Kenya. 

Edwin anasema ingawa hata yeye familia yake ilipatiwa vitisho kutokana na kazi yake, hatokata tamaa kwa kuwa kazi ndio imeanza ya kulinda wanyamapori na bayonuai kwenye mlima Kenya.