Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aina milioni 1 ya viumbe hatarini kutoweka-  Ripoti

Mbawala huyu aina ya Milu alitoweka porini mwaka 1865 kufuatia mafuriko makubwa nchini China. Kwa bahati nzuri kulikuwepo na mbawala aina hiyo waliokuwa wameshikiliwa barani Ulaya hivyo mwaka 1986 walirejeshwa tena.
UNDP China
Mbawala huyu aina ya Milu alitoweka porini mwaka 1865 kufuatia mafuriko makubwa nchini China. Kwa bahati nzuri kulikuwepo na mbawala aina hiyo waliokuwa wameshikiliwa barani Ulaya hivyo mwaka 1986 walirejeshwa tena.

Aina milioni 1 ya viumbe hatarini kutoweka-  Ripoti

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya kuhusu madhara ya shughuli za binadamu kwa mazingira inaonesha kuwa takribani aina milioni moja ya viumbe viko hatarini kutoweka ndani ya miongo kadhaa iwapo juhudi za sasa za kuhifadhi mazingira zitakwama.

Ikitolewa hii leo huko Paris, Ufaransa, ripoti hiyo iliyoandaliwa na jopo la kiserikali la masuala la sayansi na bayonuai, IPBES chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni,  UNESCO imewasilishwa mbele ya wawakilishi wa nchi 130 ili iweze kuidhinishwa.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo ya kwanza kuchapishwa tangu mwaka 2005, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema, “matokeo ya ripoti ni onyo kwa dunia. Kupitishwa kwa ripoti hii ya kihistoria, kunamaanisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayedai kuwa hakufahamu. Hatuwezi kuendelea kuharibu utofauti uliopo ambao ni wa uhai. Huu ni wajibu wetu kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

Bi. Azoulay amesema utofauti kati ya viumbe na kati ya viumbe na bayonuai ni muhimu sana duniani na suala la kulinda ni muhimu zaidi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti ikizingatia pia mikataba kama ule wa tabianchi wa Paris, inachunguza pia vichocheo vitano vya mabadiliko ya utofauti wa viumbe na bayonuia katika miaka 50 iliyopita.

Vichocheo hivyo ni mabadiliko katika matumizi ya ardhi na bahari, matumizi kupita kiasi ya viumbe, mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi na uvamizi wa viumbe vya kigeni.

Sokwe ni wanyama ambao wanazidi kutoweka kutokana na uharibifu wa makazi yao ya asili yaani msituni, nchini Uganda.
UNEP
Sokwe ni wanyama ambao wanazidi kutoweka kutokana na uharibifu wa makazi yao ya asili yaani msituni, nchini Uganda.

Kiumbe kimoja kati ya vinne kipo hatarini kutoweka

Utafiti huo  umeonesha kuwa asilimia 25 ya makundi ya wanyama na mimea wako hatarini zaidi kutoweka kutokana na shughuli za binadamu.

Kwa mantiki hiyo, “ripoti inataka hatua za dharura kulinda viumbe hivyo kwa kuwa kwa mwelekeo wa sasa takribani aina milioni Moja ziko hatarini kutoweka ndani ya miongo michache.”

Ripoti inasema kuwa licha ya hatua za mashinani, ikiwemo kutoka jamii ya watu wa asili, hadi mwaka 2016, aina 559 kati ya 6,190 za wanyama wanaofugwa majumbani na kutumika kama kitoweo na kwa kilimo, walikuwa wametoweka, ikiwa ni sawa na asilimia 9 ya idadi yote.

Usalama wa mazao nao uko hatarini

Kando na wanyama, ripoti inasema hata mazao nayo yako hatarini kutoweka na kutishia ukosefu wa uhakika wa kupata chakula.

“Kuna kupungua kwa aina tofauti za mazao ikiwemo mimea pori na hii inatishia kilimo kuwa na mnepo kwenye mabadiliko ya tabianchi,” imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa, “wakati chakula zaidi na nishati vinafikia watu kwa kiwango kikubwa hivi sasa, lakini ni kwa kuathiri uwezo wa mazingira kukidhi mahitaji ya siku za usoni.”

Uchafuzi wa bahari unatishia uwepo wa matumbawe ambayo ni muhimu kwa uhai wa viumbe vya baharini ikiwemo samaki
UNEP/Jerker Tamelander
Uchafuzi wa bahari unatishia uwepo wa matumbawe ambayo ni muhimu kwa uhai wa viumbe vya baharini ikiwemo samaki

Uchafuzi wa bahari nao umeongezeka mara 10 tangu miaka ya 1980.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ingawa uchafuzi wa hewa, maji na udongo umeendelea kuongezeka katika baadhi ya maeneo, uchafuzi wa bahari ndio umeshika kasi zaidi kwa kuwa umeongezeka mara 10 tangu miaka ya 1980.

“Uchafuzi wa bahari umeongezeka mara 10 tangu miaka ya 1980, ukiathiri aina 267 za viumbe ikiwemo asilimia 86 ya kasa, asilimia 44 ya ndege bahari na asilimia 43 ya wanyama waishio baharini,” imesema ripoti hiyo.

Ripoti hii ya 2019 ya tathmini ya bayonuai duniani ni ya kwanza pia ya aina  yake kuchunguza na kujumuisha stadi za watu wa asili katika kuhifadhi mazingira.