Idadi ya vifo vya COVID-19 duniani yafikia milioni 2,Guterres aonya ubinafsi kwenye chanjo

15 Januari 2021

Historia ya kuvunja moyo imefikiwa duniani ambapo watu milioni 2 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa utokanao na virusi vya Corona au COVID-19, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo.

Kupitia ujumbe wake aliotoa kwa njia ya video, Guterres amesema nyuma ya takwimu hizo ni majina ya watu na nyuso zao. “Tabasamu zao zimesalia historia, viti walivyokuwa wanaketi wakati wa mlo wa usiku sasa ni vitupu, na vyumba sasa vimebakia na mwangwi wa ukimya wa wapendwa wetu.”

Katibu Mkuu amesema cha kusikitisha zaidi, madhara ya janga la Corona yamekuwa mabaya zaidi kutokana na ukosefu wa juhudi za pamoja za kimataifa.

Ni kwa mantiki hiyo amesema katika kukumbuka watu hao milioni 2 waliopoteza maisha kutokana na Corona, dunia inapaswa kuchukua hatua kubwa zaidi za pamoja na kwa mshikamano.

Sasa ni wakati!

Hivi sasa chanjo salama na fanisi dhidi ya COVID-19 zinaanza kusambazwa, na Umoja wa Mataifa unasaidia nchi kuhamasisha hatua ya kihistoria ya kimataifa ya utoaji chanjo.

“Lazima tuazimie kuhakikisha kuwa chanjo hizo zinaonekana kuwa jambo jema kwa umma wa kimataifa, chanjo za watu. Hii inahitajia ufadhili kamilifu wa kufanikisha mpango wa pamoja wa kuhamasisha na kusambaza chanjo dhidi ya Corona, au COVAX ambao umejipambanua kuhakikisha kuwa chanjo zinaweza kupatiwa kila mtu,”  amesema Bwana Guterres.

Tabasamu za wapendwa wetu zimesalia kumbukumbu, viti katika meza ya mlo wa usiku vimebalia vitupu - António Guterres,  Katibu Mkuu UN

Hata hivyo amesema nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani zina wajibu wa kipekee. Ingawa hivyo hadi sasa bado kuna ombwe la kufanikisha hatua hiyo akisema kuwa, “chanjo zinafikia nchi tajiri kwa haraka zaidi, ilhali nchi maskini bado kabisa kupata chanjo hizo. Sayansi inafakiwa lakini mshikamano unakwama. Baadhi ya nchi zinaibuka na mipango yao ya kando, hata kukusanya kiwango kikubwa cha chanjo kuliko mahitaji.”

Guterres amekumbusha kuwa serikali zina wajibu wa kulinda raia wao lakini kujipendelea kwenye upataji wa chanjo ni kikwazo cha ubinafsi na kitachelewesha mpango wa dunia wa kujikwamua dhidi ya COVID-19.

Msanii akichora picha kwenye ukuta jinsi ya mbinu za mtu kujikinga dhidi ya virusi vya COVID-1 nchini Jamhuri ya afrika ya kati, CAR..
MINUSCA/Screenshot
Msanii akichora picha kwenye ukuta jinsi ya mbinu za mtu kujikinga dhidi ya virusi vya COVID-1 nchini Jamhuri ya afrika ya kati, CAR..

COVID-19 haiwezi kutokomezwa na nchi moja pekee

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa utokomezaji wa COVID-19 hautawezekana iwapo kila nchi itachukua hatua ya peke yake. Hivyo inahitajika watengenezaji wa chanjo kuongeza azma yao ya kushirikiana na COVAX na nchi zote duniani ili kuhakikisha kuna usambazaji sawia na wa kutosheleza.
Amesema nchi zinahitajika kuazimia kusambaza dozi za ziada za chanjo kwa nchi nyingine na hiyo itasaidia kupatia chanjo wahudumu wa afya kwa misingi ya udharura na kulinda mifumo ya afya isisambaratike.

Amekumbusha kuwa wahudumu wengine walio mstari wa mbele pamoj ana wafanyakazi wa kibinadamu na watu walio hatarini zaidi lazima nao wapatiwe kipaumbele katika utoaji wa chanjo.

Kuhusu imani ya umma kwa chanjo inayotolewa, Katibu Mkuu amesema ni lazima kutumia njia fanisi za mawasiliano na kusambaza ufahamu na uelewa wake, ili kujenga imani ya wananchi kwenye chanjo hiyo.

Amesema wakati sayansi inaendelea kufungua njia mpya za matumaini, “tukumbuke njia rahisi zaidi za kuhakikisha kila mtu yuko salama: vaa barakoa, epuka kuchangamana na mikusanyiko.”

Guterres amesema umoja ndio njia pekee ya kuondoka dunia dhidi ya janga la Corona kwa kuwa, “mshikamano wa dunia utaokoa maisha, utalinda wat una kusaidia kushinda virusi hatari vya Corona.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter