Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 ni kengele ya kujiandaa vyema dhidi ya majanga- Guterres

Muuguzi akiwa amevalia barakoa anampatia huduma ya kwanza mtoto mchanga aliyezaliwa kwenye kituo cha afya cha Port Bouet, kilichoko katika viunga vya mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.
© UNICEF/UNI312809// Frank Dejongh
Muuguzi akiwa amevalia barakoa anampatia huduma ya kwanza mtoto mchanga aliyezaliwa kwenye kituo cha afya cha Port Bouet, kilichoko katika viunga vya mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.

COVID-19 ni kengele ya kujiandaa vyema dhidi ya majanga- Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kujindaa dhidi ya majanga yamekuja katika kipindi ambacho ni muafaka na kuakisi kile ambacho kinapaswa kufanywa ili kuepuka madhara makubwa.

Guterres amesema hayo katika ujumbe wake wa siku hiyo inayoadhimishwa hii leo, ikiwa ni mara ya kwanza kabisa, maadhimisho yakifanyika huku janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 likiwa limeshasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 1.7.

“Maadhimisho haya ya kwanza ya siku ya kimataifa ya kuijndaa kukabili majanga yameagukia mwisho wa mwaka katika hali ambayo wengi walihofia na imetokea ni kweli ya kutisha”, amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema COVID-19 imesababisha vifo, chumi zimesambaratika, jamii zimetibuliwa na kutumbukiza walio hatarini katika hali mbaya zaidi kuwahi kutokea.

“Tunapohaha kudhibiti na kujikwamua kutoka katika janga la sasa, tunapaswa kufikiria siku za usoni. Bahati mbaya ni rahisi kufikiria virusi ambavyo vinaambukiza zaidi lakini hatari zaidi”, amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa tayari tunaweza kujifunza kutokana na uzoefu wa mwaka jana.

Muuza nyama akiwa amevalia barakoa yake katika duka lake la nyama huko sokoni KonyoKonyo mjini Juba ,nchini Sudan Kusini.
UNICEF/Bullen Chol
Muuza nyama akiwa amevalia barakoa yake katika duka lake la nyama huko sokoni KonyoKonyo mjini Juba ,nchini Sudan Kusini.

Kujiandaa ni uwekezaji bora zaidi, unaogharimu fedha kidoog kulinganisha na gharama za dharura. “Jamii zinahitaji mifumo thabiti ya afya, ikiwemo huduma ya afya kwa wote. Nchi zinahitaji hifadhi zaidi ya kijamii. Jamii zilizo mstari wa mbele zinahitaji usaidizi. Nchi zinahitaji msaada fanisi zaidi wa kiufundi”, amesema Katibu Mkuu.

Uhusiano wa binadamu na wanyama

Amekumbusha kuwa tunahitaji kuangazia zaidi muingiliano wa binadamu na mifugo katika makazi ya wanyama akisema kuwa asilimia 75 ya magonjwa mapya na yanayoibuka ya kuambukiza yana uhusiano na wanyama.

Amesema katika hali hiyo, sayansi lazima iwe mwongozo. Mshikamano na uratibu ni muhimu ndani na baina ya nchi kwa kuwa hakuna aliye salama hadi kila mmoja yu salama.

Tujiandae vyema

Bwana Guterres amesema mfumo wa Umoja wa Mataifa, likiwemo shirika lake la afya, WHO uko thabiti katika kusaidia serikali na wadau wote katika kuimarisha maandalizi dhidi ya magonjwa ya milipuko kama ikiwemo sehemu ya kazi yao kubwa ya kujenga dunia yenye afya na hivyo kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Siku ya kimataifa ya kujiandaa dhidi ya majanga imeangukia tarehe ya kuzaliwa Louis Pasteur, mwanabailojia wa kifaransa ambaye aligundua chanjo. Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema, “katika kutambua kazi yake, napongeza wataalamu wa kitabibu, wafanyakazi wa afya ambao wameipitisha dnia katika kipindi hiki kigumu cha dharura kwa mchango wao wa kipekee.”

Ametamatisha ujumbe wake akisema kuwa tunapojikwamua kutoka katika janga hili, hebu na tuazimie kujenga uwezo wetu wa kujikinga ili tuwe tayari pale dunia itakapokabiliwa na mlipuko mwingine.