Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zinazoendelea zaongoza kwa idadi ya watu wenye utipwatipwa

Chakula chenye virutubisho vya kutosha vya lishe kinaweza kumwondoa mtu hususani watoto katika hatari ya kupata magonjwa.
World Bank/Maria Fleischmann
Chakula chenye virutubisho vya kutosha vya lishe kinaweza kumwondoa mtu hususani watoto katika hatari ya kupata magonjwa.

Nchi zinazoendelea zaongoza kwa idadi ya watu wenye utipwatipwa

Afya

“Katika siku hii ya afya ya mmeng’enyo wa chakula duniani, kwa pamoja tujilotee kushirikiana kutatua tatizo la utipwatipwa kwa mustakabali wa ulimwengu endelevu na wenye afya.” 

Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya afya ya mmeng’enyo duniani. 

Katibu mkuu  amewataka watu wote ulimwenguni kushiriki kupunguza tatizo hilo la unene uliopitiliza.
Katika ujumbe huo uliotolewa mjini New York Marekani, Guterres amesema dunia inashuhudia kuongezeka kwa janga la utipwatipwa tatizo ambalo amesema“Linaathiri watu wa rika zote kutoka pembe zote za ulimwengu. Hali hii inaogofya zaidi inavyo athiri vijana. Katika miongo 4 iliyopita, asilimia ya watu wenye umri kati ya miaka 5-19 ambao wana unene uliopitiliza au utipwatipwa imeongezeka zaidi ya mara nne, kutoka asilimia 4 mpaka asilimia 18. Duniani, zaidi ya watu milioni 4 wanakufa kila mwaka kutokana na uzito uliopitiliza au utipwatipwa.”

Ameongeza kuwa awali tatizo lilikuwa likionekana kwenye nchi zilizo endelea, lakini sasa unene uliopitiliza na utipwatipwa  unaongezeka zaidi kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati, hususan sehemu za mijini.
“Idadi kubwa ya watoto wenye utipwatipwa au unene uliopitiliza wanaishi kwenye nchi zinazo endelea, ambapo kasi ya kuongezeka kwa tatizo imekuwa kwa asilimia 30 ikilinganishwa na nchi zilizoendelea.” 

Janga la Corona au COVID-19 limeonesha ni namna gani tatizo hili la utipwatipwa ni hatari kwa afya, kwa kuwa watu wenye unene uliopitiliza wapo kwenye hatari mara nne zaidi ya kupata madhara makubwa zaidi ya ugonjwa wa Corona. 
“Baraza la afya duniani limeweka malengo ya kupambana na utipwatipwa kwa watoto, barubaru na watu wazima ifikapo mwaka 2025. Kwa kiwango kilichopo sasa hivi, hakuna lengo hata moja linalo onekana linaweza kufikiwa, ilihali utipwatipwa na shida zake zinazoweza kuepukwa” unaongezeka amesema Guterres. 


 Nini kifanyike?
Guterres amesema, 
•    Kwanza, tunahitaji kujikinga, kwa kuanzia na mlo wenye lishe nzuri wakati wa ujauzito, ikifuatiwa na unyonyeshaji pekee kwa mtoto katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya maisha yake, na kuendelea kumnyonyesha mpaka afikie miaka 2 na kuendelea. 
•    Pili, tunahitaji sera na uwekezaji ambao utarahisisha upatikanaji wa chakula bora na chenye lishe, jambo ambalo linapashwa kuelezwa kwenye mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya chakula.
•    Tatu, watu wenye unene kupita kiasi na pitwapitwa wanapaswa kupata huduma bora kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.