Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaingilia kati kuokoa watoto Korogocho Kenya 

Picha ya juu ikionesha mtaa wa mabanda wa Mathare mjini Nairobi Kenya. Mitaa hii haina tofauti sana na mitaa mingine jirani ya mabanda kama Korogocho.
UN-Habitat/Julius Mwelu
Picha ya juu ikionesha mtaa wa mabanda wa Mathare mjini Nairobi Kenya. Mitaa hii haina tofauti sana na mitaa mingine jirani ya mabanda kama Korogocho.

UNICEF yaingilia kati kuokoa watoto Korogocho Kenya 

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, kwa msaada wa shirika la Uingereza, UK Aid, linasaidia kutoa huduma ya ulinzi kwa watoto katika makazi  duni au yasiyo rasmi, Korogocho, walioathiriwa na kufungwa kwa shule kutokana na janga la COVID-19.

Korogocho, Kenya, eneo la makazi duni lenye ukubwa wa kilomita moja na nusu za mraba na idadi ya watu inayokadiriwa kufikia laki mbili. 

Kama ilivyokuwa kwa maeneo mengine duniani, watoto wa Korogocho nao wamelazimika kubaki nyumbani kutokana na kuzuka kwa janga la virusi vya corona. Athari hazijaishia tu katika kukosa masomo bali pia wamekumbana na unyanyasaji kama anavyoeleza mtoto huyu mwenye umri wa miaka 7, amepewa jina Kijana, ili kuhifadhi jina lake halisi. Mtoto huyu anasema, “nilikuwa ninacheza mchezo wa kujificha na kufichuana wakati vijana wawili waliponiita, wakanivua nguo kisha waakanza kunivuta (sehemu zangu za siri). Kisha wakanipiga. Nilikuwa nasikia uchungu. Nilienda haja ndogo nikasikia uchungu. Nikarudi nikamwambia mama akanipeleka hospitali.” 

Kesi ya mtoto huyu ilifikishwa katika Idara ya huduma za watoto na polisi baada ya kuwa amepatiwa matibabu, lakini vijana waliomfanyia unyanyasaji hawakupatikana. 

Eugenia Olliaro ni afisa wa UNICEF katika kitengo cha ulinzi wa watoto katika dharura anasema wakati wa kufungwa kwa shule wameona ongezeko la unyanyasaji dhidi ya watoto ukiwemo unyanyasaji wa kingono na kijinsia. Matukio haya ni theluthi ya matukio yote ya uhalifu yaliyoripotiwa nchini Kenya tangukuanza kwa COVID-19

UNICEF kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la TDH linalopigania haki za watoto, wamefadhili mafunzo ya washauri jamii 130 ndani ya Kogorogo. Hawa wanaripoti matukio ya unyanyasaji kwa walinzi wa watoto au polisi. Margaret Mbala ni mmoja wa washauri hao, anasema, “nilikuja kuwa mshauri jamii. Kwa sababu ninapenda mahali ninapoishi. Na nilipokuwa naona watu wanafanya makosa kwa sababu hawajui, TDH walinichukua wakanipeleka kwenye mafunzo, wakanifunza vile ambavyo ninaweza kufundisha hata wale wengine mbao hawakuwa wanajua kuwa wanakosea, sasa nilianza kuwafunza ili wasije wakafanya tena makosa mengine ambayo yanaweza kuja kuwadhuru baadaye.”