Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa unafanya juhudi za kuhakikisha uwepo wa amani, CAR ikienda kwenye uchaguzi. 

MINUSCA wametuma vikosi vya polisi katika mji mkuu wa CAR, Bangui na viunga vyake kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na makundi yenye silaha kaskazini magharibi mwa mji.
MINUSCA/Hervé Serefio
MINUSCA wametuma vikosi vya polisi katika mji mkuu wa CAR, Bangui na viunga vyake kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na makundi yenye silaha kaskazini magharibi mwa mji.

Umoja wa Mataifa unafanya juhudi za kuhakikisha uwepo wa amani, CAR ikienda kwenye uchaguzi. 

Amani na Usalama

Msemaji wa Katibiu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephan Dujarric akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini New York Marekani kuhusu yaliyojadiliwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, amesema Baraza hilo limejadili kuhusu hali ya kukosekana kwa usalama ncini Jamhuri ya Afrika ya kati huku nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi. 

Kwa mujibu wa Dujarric, ‘Muungano wa vikundi vyenye silaha’ katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ulifanya mashambulio ya mfululizo na kujaribu kufikia mji mkuu Bangui wakati mivutano ya kisiasa na usalama ikiongezeka kabla ya uchaguzi wa nchi hiyo.  

Bwana Dujarric ameeleza kuwa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA, umeripoti kuwa hali ya wasiwasi ya kisiasa na kiusalama imeongezeka mwishoni mwa wiki katikati mwa kampeni za uchaguzi zinazoendelea ili kupata Rais na wabunge. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 27 ya mwezi huu wa Desemba. 

Amesema vikundi vyenye silaha, "wakati huo huo vilishambulia wilaya nne katika maeneo ya magharibi na kusini mwa nchi na kujaribu kwenda mji mkuu Bangui. Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walijibu mashambulizi katika maeneo kadhaa. Hakuna uharibifu wowote ulioripotiwa.” 

Jumapili, MINUSCA na wanachama wa kikundi cha G-5 kilicho na washirika wakuu wa kimataifa katika CAR walifanya mkutano kulaani matukio hayo na kutoa wito kwa wadau kuacha vurugu. Walielezea pia kuunga mkono kwao kufanyika kwa uchaguzi kama ilivyopangwa. 

Aidha msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, “tutaendelea kushirikiana na wadau wote katika juhudi za kupunguza mivutano, kuhimiza vyama kutatua shida zao kupitia njia za amani na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa."