Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanafunzi wenye ulemavu Malawi waelimishwa kuhusu COVID-19 

Wanafunzi nchini Malawi wenye ulemavu wakifuatilia darasa kuhusu ugonjwa wa COVID-19.
UNICEF Malawi Video capture
Wanafunzi nchini Malawi wenye ulemavu wakifuatilia darasa kuhusu ugonjwa wa COVID-19.

Wanafunzi wenye ulemavu Malawi waelimishwa kuhusu COVID-19 

Afya

Janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19 likiendelea kushika kasi katika baadhi ya nchi, Umoja wa Mataifa nao kupitia shirika lake la kuhudumia watoto UNICEF nchini Malawi pamoja na wadau, wamechukua hatua kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika kupata elimu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Ndani ya darasa la watoto wenye ulemavu nchini Malawi, mwanafunzi wa darasa la 4 Wyson Simon mwenye ulemavu wa kutoona, akisoma kutoka kwenye daftari lenye alama za nukta nundu. 

Anasema hebu tutokomeze COVID-19

Wanafunzi hawa wanaelimishwa kuhusu COVID-19 na mbele ya darasa ni mwalimu akiwa amevalia barakoa na kiziba uso akitumia lugha ya alama na sauti kuhakikisha wanafunzi viziwi nao wanafuata kile Wyson anachosoma. 

Wyson anaendelea kufafanua kuwa, COVID-19 ni jina la ugonjwa unaosababishwa na virusi aina ya Corona. Dalili za mtu mwenye COVID-19 ni homa, kikohozi, kushindwa kupumua, na pia kupumua haraka.  

Anaendelea kusema kuwa kumbuka mtu anaweza kuanza kusambaza virusi vya Corona hata kabla ya dalili kuanza kuonekana.  

Akaendelea kutumia kitabu chenye maandishi ya nukta nundu kuelezea jinsi COVID-19 inasambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine na kisha anamalizia na namba ya simu ambayo mtu anaweza kuipiga ili kupata msaada zaidi. 

Kisha mwalimu akitumia lugha ya alama akauliza wanafunzi maswali kama vile jinsi COVID-19 inasambazwa,  ili kubaini iwapo wameelewa au la!    

Wanafunzi walijibu!  

Na mwalimu akawapatia msisitizo kwa sauti na alama! 

Mwalimu anakumbusha, epuka kukaribiana, zingatia umbali! Salia nyumbani! Shukrani na huu ndio mwisho wa darasa letu! 

 Ama hakika wa wanafunzi walielewa vyema.!