COVID-19 limepunguza huduma na ulinzi kwa wahamiaji na watoto waliotawanywa:UNICEF

18 Disemba 2020

Takwimu za utafiti mpya uliochapishwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF zinaonyesha kwamba katika nchi zote duniani wahamiaji na watoto waliotawanywa hawahusishwi katika hatua za kitaifa za kupambana na kujikwamua na janga la corona au COVID-19 na wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa fursa za huduma muhimu. 

Matokeo yaliyopatikana baada ya UNICEF kukusanya tawili katika utafiti huo wa karibuni kabisa kwenye 159 zilizo na operesheni za shirika hilo yanakadiria kwamba milioni mwa wahamiaji wa kimataifa milioni 272 kote duniani , milioni 33 kati yao ni Watoto, wakiwemo Watoto wakimbizi milioni 12.6 na waomba hifadhi milioni 1.5. 

Na wengine kwa mamilioni wanakimbia na kuhama ndani ya nchi zao. Mathalani utafiti huo unasema “India pekee inahifadhi Watoto wahamiaji wa ndani milioni 93  na kote duniani Watoto milioni 21.5 wamekuwa wakimbizi wa ndani kutokana na vita, machafuko au majanga.” 

Siku ya wahamiaji 

Na leo ikiwa siku ya kimataifa ya wahamiaji UNICEF imezitaka serikali kuhakikisha kwamba Watoto wote walio hatarini wakiwemo wanaoishi kama wakimbizi, wahamiaji au wakimbizi wa ndani wanapewa kipaumbe katika hatua za kukabiliana na juhudi za kujikwamua na COVID-19 bila kujali hadhi zao na kuwafikia na huduma za ulinzi, huduma za afya, maji, usafi na elimu. 

“Matokeo ya utafiti huu yanamulika taa nyekundu yakitahadharisha kwamba watoto walio hatarini zaidi wanaachwa peke yao kukabiliana na athari za COVID-19” amesema mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore na kuongeza kuwa “Kwa msaada sahihi na kwa wakati muafaka watoto wanaohama au kukimbia makwao wanaweza kuchangia ujuzi muhimu kwenye makazi yao mapya, ujuzi ambao nchi zinapaswa kuutumia kujikwamua na COVID-19. UNICEF inatoa wito wa uwekezaji zaidi wa kimataifa kuwasaidia watoto hawa na kuwa tayari kushirikiana na serikali ili kufikia faida bora ambazo zinaletwa na Watoto wahamiaji.” 

Utafiti huo unaonyesha kwamba upunguaji mkubwa wa huduma unafanyika kwenye nchi zilizo na migogoro inayoendelea kama vita au majanga, ambako Watoto walio mbiloni tayari walikuwa wanakabiliwa na vikwazo vya kupata fursa za huduma za afya, maji safi na huduma za kujisafi. 

Kilichobainiwa na utafiti 

Kwa mujibu wa utafiti huo katika asilimia 50 ya nchi ambako UNICEF inaendesha operesheni zake za kibinadamu kuna upungufu wa fursa za huduma za afya miongoni mwa watu waliotawanywa na wakimbizi. 

Na karibu robo ya nchi hizo zimefripoti kuvurugwa kwa huduma za maji, usafi na kujisafi katika makambi ya wakimbizi na watu waliotawanywa.  

Pia takwimu za utafiti huo zinaonyesha kwamba wakimbizi, wahamiaji na Watoto waliotawanywa hawafikiwi kama sehemu yah atua za kijamii na kiuchumi za kujikwamua na janga hilo. Mfano  

  • Asilimia 58 ya nchi zilizofanyiwa utafiti na UNICEF kumeripotiwa ufungufu wa huduma za kusomea majumbani kwa Watoto wajiojiweza wakiwemo wanaoishi kama wakimbizi, wahamiaji na wakimbizi wa ndani. 
  • Asilimia 36 wameripoti kupungua kwa huduma za ulinzi kwa Watoto wahamiaji na waliotawanywa.  
  • Na asilimia 50 wameripoti kwamba wakimbizi na waomba hifadhi hawahusishwi katika hatua mpya au zilizoongezwa za COVID-19 ambazo zinachukuliwa na serikali katika ulinzi wa hifadhi ya jamii. 

Hofu ya UNICEF

UNICEF pia inatiwa mashaka kuhusu ongezeko la mtazamo hasi na ukatili dhidi ya watoto wahamiaji, mwenendo unaotarajiwa kushika kasi hasa athari za kiuchumi na kijamii zilizoletwa na COVID-19 zikiongezeka na mamilioni ya wahamiaji wakirejea nyumbani katika nchi ambazo kiwango cha ukosefu wa ajira kinaongezeka. 

Pia utafiti huo umebaini kwamba asilimia 39 ya nchi zilizofanyiwa utafiti kuna ongezeko la mivutano dhidi ya wahamiaji na watu waliotawanywa Pamoja na wanaorejea hali ambayo inaongezeka hadi karibu asilimia 50 kwa nchi zilizo katika hali mbaya. 

UNICEF inashirikiana na wadau wengine kuwasaidia wahamiaji na watu waliotawanywa kujilinda dhidi ya COVID-19 na athari zake. Na hii inajumuisha kuwapa taarifa sahihi na Rafiki kwa Watoto kuhusu COVID-19 na hatua za kujisafi kwa lugha wanayoielewa, kuhakikisha wanapata fursa ya usafi na maji popote walipo na kuhakikisha kwamba wahamiaji na watu waliotawanywa hawaachwi nyuma katika juhudi za kuhakikishiwa fursa za elimu, afya, lishe na huduma za ulinzi kwa watoto. 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter