Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majimbo Brazil yaibuka na mbinu bunifu ili kila kaya iwe na mfumo wa majitaka 

Kijana nchini Brazil
Agência Brasil/Marcelo Camargo
Kijana nchini Brazil

Majimbo Brazil yaibuka na mbinu bunifu ili kila kaya iwe na mfumo wa majitaka 

Afya

Nchini Brazil majimbo ya Espirito Santo na Sao Paulo yanaendesha kampeni mahsusi kuhakikisha kuwa kila nyumba inakuwa imeunganishwa na mfumo wa majitaka ili kaya hizo ziweze kunufaika na matumizi ya mifumo ya aina hiyo ambayo ni pamoja na kuepusha magonjwa.

Mifumo ya kupitisha majitaka imepanuka katika nchi za kipato cha chini na kati duniani kote, lakini bado nyumba nyingi hazijaunganishwa na mifumo hiyo hata kama imepita mbele ya nyumba zao.  

 

Matokeo yao, si wao wala miji ambamo wanaishi, wananufaika na faida za kiafya, kiuchumi na kimazingira za uwepo wa huduma hizo.  

Ni kwa mantiki hiyo kampuni za huduma za majitaka, serikali na wadau wao wanachukua hatua kuhakikisha kaya zina huduma hizo.  

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia,  majimbo ya Espirito Santo na Sao Paulo nchini Brazil, yamepitisha sheria ambapo ni  lazima kila nyumba iunganishwe katika mfumo wa majitaka. Hata hivyo nyumba nyingine zimeshindwa kwa kuwa zenyewe ndani hazina mfumo wa majitaka, wamiliki hawana fedha au hata hawatambui umuhimu.  

Kupitia kampeni Jiunge katika Mtandao, kampuni za majitaka kwenye majimbo hayo zinatoa huduma bure za kufunga mfumo wa majitaka ndani ya nyumba na kisha unapokamilika, mmiliki anaanza kulipa ankara za maji.  

Dante Ragazi Pauli ni afisa wa kampuni ya majitaka ya Sao Paulo,  « Tunaingia nyumba ya mteja na kufanya maandalizi yote ili mtu huyu mwenye kipato kidogo aweze kufunga mfumo wa majitaka bila malipo yoyote. Kisha anaweza kuunganishwa kwenye mfumo wa manispaa wa majitaka. Hapo unajikuta umehudumia watu ambao hatimaye watalipa ankara za maji .Na kweli kaya zinalipa ankara zao kwa wakati.»  

Maria Diaz ni mmoja wa wanufaika jimboni Sao Paulo.  «Tunalipa kiwango cha chini, na iwapo ukitumia zaidi basi unalipa zaidi. Ni jambo zuri sasa hivi watoto hawarandirandi kwenye majitaka, ambako wangepata maambukizi. Hali ya maisha imekuwa bora.