Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasiwasi waenea kuhusu ukatili dhidi ya watoto na utekaji Afrika Magharibi na Afrika ya kati-UNICEF

Watoto waliofurushwa Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
© UNICEF/Olivia Acland
Watoto waliofurushwa Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Wasiwasi waenea kuhusu ukatili dhidi ya watoto na utekaji Afrika Magharibi na Afrika ya kati-UNICEF

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeelezea wasiwasi wake kufuatia tukio la hivi karibuni la watoto 150 kuripotiwa kutekwa  wakiwa wanatoka shuleni katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria. 

UNICEF inasema tukio hilo la tarehe 5 mwezi huu wa Julai ni moja ya matukio ya mfululizo wa ukatili dhidi ya watoto na utekwaji nyara ikiwemo wanafunzi katika maeneo ya Afrika Magharibi na Kati. 

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore iliotolewa leo jijini New York, Marekani imesema ana wasiwasi kwamba katika miaka iliyopita makundi yaliyojihami na wadau katika mizozo nchini Burkina Faso,  

Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC, NIger na Nigeria yataongeza matukio hayo ya ukatili katika kipindi cha wiki chache zijazo kuelekea msimu wa mvua ambapo safari zitadhibitiwa kufuatia mafuriko.  

Bi Fore amesema, “matukio kama hayo yanaonekana kuongezeka na hivyo kuongeza hofu kuhusu usalama wa watoto katika ukanda huo. Tayari mwaka 2020, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa  

Mataifa kuhusu watoto kwenye mizozo ya silaha, mtoto mmoja kati ya watatu aliyekabiliwa na ukatili mkubwa alikuwa Afrika magharibi na Afrika ya Kati.”  

Akitolea mfano baadhi ya matukio ya ukatili, Bi Fore ametaja Burkina Faso, ambako mashambulizi dhidi ya raia na ukiukwaji wa haki za kibinadamu za  kimataifa yameongezeka katika wiki chache ziilizopita.  

Mnamo tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu, takriban watu 130 waliuawa baada ya kijiji kushambuliwa jimboni Yagha. Hiyo ni moja ya mashambulio 

 yaliyosababisha vifo vingi nchini humo tangu kulipuka kwa mzozo mnamo 2015.   

UNICEF imesema, “nchini Nigeria Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba  takriban wanafunzi 950 wametekwa nyara kutoka shule zao na watu waliojihami tangu Desemba mwaka jana. Katika kipindi cha wiki sita pekee  takriban watoto 500 walitekwa nyara katika matukio manne tofauti katika maeneo ya kati na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Wengi wa watoto hao bado hawajarejea nyumbani. Ni vigumu kuelewa uchungu na hofu ya familia na jamaa wakati wa kutokuwepo kwao.”  

Halikadhalika Bi. Fore ameongeza, “nchini DRC katika robo ya mwaka 2021 pekee, zaidi ya ukatili aina 3,400 dhidi ya watoto ikiwemo kusajiliwa katika makundi yaliyojihami, utekwaji na mauaji vilithibitishwa ikiwa ni asilimia 64 ya jumla ya ukatili uliothibitishwa mwaka wa 2020.”  

UNICEF imesema haitoshi kulaani uhalifu huo wakati mamilioni ya watoto wanakabiliwa na janga la hali inayozorota ya ulinzi. Watoto wanaoishi katika maeneo hayo wanahitaji juhudi za pamoja kuhakikisha kwamba wanaishi katika maeneo salama, kuhudhuria shule na kuchota maji bila hofu ya kushambuliwa au kuchukuliwa kutoka kwa familia zao.  

Kwa mantiki hiyo Bi. Fore amesema, la kwanza ni makundi yaliyojihami na wadau katika mizozo wanaotekeleza ukatili dhidi ya haki za watoto  

kuhakikisha wanasitisha mashambulizi dhidi ya raia na kuheshimu na kulinda raia na mali zao wakati wa operesheni za kijeshi.  

Aidha jamii ya kimataifa ina wajibu muhimu, “tunahitaji wafadhili kuongeza ufadhili ili tuweze kupanua wigo wa kazi zetu na kupunugza hatari ya watoto na kuwajengea mnepo ili kuhakikisha usalama wao. Juhudi hizo ni pamoja na kuweka mazingira ya muda salama katika maeneo ambako shule zimefungwa kwa ajili ya ukosefu wa usalama, kutoa huduma za kisaikolojia na kijamii kwa watoto walioathiriwa na ukatili na kuunga mkono elimu juu ya uelewa wa hatari za migodi.”  

Bi. Fore amehitimisha kwa kusema, “kila juhudi inahitajika kubadili hali ya sasa janga la usalama wa watoto kwani ukanda uko katika hatari ya janga kubwa.”