Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ili kufanikisha malengo yetu lazima tuwajumuishe watu wenye ulemavu:UN

UNDP inatoa msaada wa dharura kwa ajili ya kuzuia corona kenye maeneo ya watu masikini mijini nchini Bangladesh
UNDP/Fahad Kaizer
UNDP inatoa msaada wa dharura kwa ajili ya kuzuia corona kenye maeneo ya watu masikini mijini nchini Bangladesh

Ili kufanikisha malengo yetu lazima tuwajumuishe watu wenye ulemavu:UN

Haki za binadamu

Kuwa na dunia ambayo watu wote wana uwezo wa kupata fursa saw ani lengo ambalo linastahili kupiganiwa amesema Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa katika hotuba yake hii leo akitoa wito wa ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika jamii ikiwemo katika hatua za kukabiliana na kujikwamu na janga la corona au COVID-19.

Hotuba hiyo ameiwasilisha kwa njia ya mtandao katika ufunguzi wa mkutano wa nchi wanachama wa mkataba wa 2006 wa haki za watu wenye ulemavu.

Guterres amesisitiza kwamba mkataba huo unaweza tu kutekelezwa kikamilivu kwa kushughulikia vikwazo, ukiukwaji wa haki na ubaguzi unaowakabili watu wenye ulemavu.

“Kutambua haki za watu wenye ulemavu ni muhimu katika kutimiza ahadi ya ajenda ya maendeleo ya 2030 ya kutomwacha yeyote nyuma.” Akimaanisha hatua za kimataifa zenye lengo la kuifanya dunia kuwa endelevu na yenye haki zaidi.

“Katika hatua zetu zote lengo ni bayana kuwa na dunia ambayo watu wote wanafurahia fursa sawa, wanashiriki katika ufanyaji maamuzi na kufaidika kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni. Hilo ni lengo linalostahili kulipigania.”

COVID-19 imeongeza pengo la usawa

Kikao cha 13 (COSP13) cha mkutano wa nchi wanachama wa mkataba wa mkataba wa watu wenye ulemavu kimeanza siku chache kabla ya maadhimisho ya siku ya kimataigfa ya watu wenye ulemavu ambayo hufanyika kila mwaka Desemba 3.

Kama ilivyo matukio mengi mwaka huu kinafanyika kikighubikwa na kivuli cha janga la COVID-19 huku washiriki wakihudhuria uso kwa uso na asilimia kuwa mtandaoni.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa janga hili limepanua pengo la usawa ambalo lilikuwepo na ambalo linawaathiri watu bilioni moja wenye ulemavu duniani.

Guterres amesema hata katika mazingira ya kawaida bila COVID-19 watu hawa ndio wengi waliokuwa wakikosa fursa za elimu, huduma za afya na ajira au kujumuishwa katika jamii zao.

Safari bado ni ndefu

Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu akiunga kauli hiyo ya katibu Mkuu, Danlami Umatu Basharu amesema anatiwa hofu kubwa na vikwazo vya kimuundo, kutojumuishwa na hali ya ubaguzi ambayo imeongezeka sana wakati wa janga hilo la COVID-19.

“Wakati nikifurahia kwamba sasa kuna wanachama 182 katika mkataba huu, COVID-19 imeanika wazi Ushahidi kwamba bado kuna safari ndefu ya kuelewa kikamilifu muundo wa haki za binadamu za watu wenye ulemavu zilizojumuishwa katika mkataba huo na hivyo kutekelezwa kikamilifu kama unavyopaswa.”

Mwezi Mei mwaka huu Katibu Mkuu alitoa tamko la kisera likiainisha athari kubwa na mbaya za COVID-19 kwa watu wenye ulemavu.

Mustakbali uwe jumuishi

Guterres ametoa wito kwa hatua za kukabiliana na COVID-19 na kujikwamua na janga hilo kujumuisha wwatu wenye ulemavu zikianzia na kutambua na kulinda haki za binadamu za watu wenye ulemavu.

“Lazima pia tuhakikishe kwamba maono na matarajio ya watu wenye ulemavu yanajumuishwa na kutambuliwa katika mikakati ya baada ya COVID-19.”

Katibu Mkuu akaenda mbali zaidi na kusisitiza kwamba kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu ni muhimu na lazima kwa ajili ya kudumisha maadili na misingi inayounda Umoja wa Mataifa.