Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani Sudan Kusini watumia njia bunifu kufadhili elimu ya watoto 

Wanafunzi katika shule ya Exodus Academy nchini Sudan Kusini.
UNIFEED/UNMISS/Video capture
Wanafunzi katika shule ya Exodus Academy nchini Sudan Kusini.

Walinda amani Sudan Kusini watumia njia bunifu kufadhili elimu ya watoto 

Utamaduni na Elimu

Timu ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumia Sudan Kusini wanatafuta njia za ubunifu za kutafuta pesa za kulipia ada ya watoto yatima na watoto katika familia zenye mzazi mmoja, kutoa chakula, vitabu na kuboresha vyumba vya madarasa vya shule ambayo inahudumia jamii maskni katika mji mkuu Juba. 

Bendera ya Sudan Kusini inapepea juu ya shule ndogo katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Paa la vyumba vya madarasa limepandishwa na vipande vya miti na kuna madawati machache. Licha ya upungufu mkubwa wa mazingira haya ya kujifunzia, angalau kwa hatua hii ni maboresho makubwa ikilinganishwa na hali iliyokuwa miaka michache iliyopita ambapo wanafunzi walilazimika kusomea nje. Sokiri George ni Mkuu wa shule hiyo ya Exodus Academy anasema, “Imekuwa ni changamoto kubwa sana tangu mwanzo kwa sababu tulianza kuanzia mwanzo. Hakukuwa na vyumba vya madarasa. Watoto walikuwa wanajifunza chini ya miti. Wengine walikuwa wanakaa kwenye mavumbi. Hakuna vitabu sahihi vya kufundishia na hata wanafunzi wenyewe hawakuwahi kuwa na vitabu vya kuandika.” 

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS una makazi karibu na shule hiyo. Kwa miaka michache iliyopita, walinda amani wametoa msaada wowote wanaoweza ukiwemo uwanja wa michezo, maji, vitabu, madawati na mengine kama hayo. Mpango wa hivi karibuni ni utengenezaji na uuzaji wa kitabu maalum kwa kutumia picha na nukuu za kuhamasisha kutoka kwa watoto ili kupata pesa za kulipia ada ya watoto yatima na watoto katika familia za mzazi mmoja, kutoa chakula, vitabu na kuboresha vyumba vya madarasa. 

Mlinda amani wa Australia Kapteni Stephanie Palfrey-Sneddon ndiye anayeongoza mradi huo ambao ameongoza pamoja na majukumu yake rasmi kama afisa wa wafanyakazi katika Kituo cha operesheni za pamoja cha UNMISS, anasema, “Kuufanyia kazi Umoja wa Mataifa imekuwa ni ndoto yangu kwa muda mrefu sana. Lakini kufanya kazi kwa shirika kubwa kama hilo wakati mwingine inakufanya kuhisi kama hatuwezi kufikia watu ambao tuko hapa kufanya kazi pamoja nao. Kwa hivyo, kuweza kuhusika katika jamii, kufanya urafiki na waalimu, wafanyakazi na kupata lulu za busara kutoka kwa baadhi ya wanafunzi imekuwa ishara kuu ya wakati wangu Sudani Kusini. " 

Timu hii ya walinda amani inaangalia ni jinsi gani wanaweza kuendelea kuwasaidia watoto hawa kufikia uwezo wao wote na kutoa mchango katika kuijenga nchi yao baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.