Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani watu wenye silaha kushambulia na kuua raia, Maiduguri, Nigeria. 

Fati Yahaya alikimbilia Cameroon kutokana na makundi ya kujihami Nigeria
UN Photo/Eskinder Debebe)
Fati Yahaya alikimbilia Cameroon kutokana na makundi ya kujihami Nigeria

UN yalaani watu wenye silaha kushambulia na kuua raia, Maiduguri, Nigeria. 

Amani na Usalama

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Nigeria, Edward Kallon ameeleza kukasirishwa na kusikitishwa na shambulio dhidi ya raia lililotekelezwa na vikundi visivyo vya serikali vyenye silaha katika vijiji vya mji mkuu wa Borno, Maiduguri. 

"Makumi ya raia wameauawa bila huruma na wengine wengi wamejeruhiwa katika shambulio hili." Ameeleza Bwana Kallon kupitia taarifa iliyosambazwa hii leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya Umoja wa Mataifa OCHA nchini Nigeria. 

Taarifa imeeleza kuwa mwanzoni mwa alasiri ya Novemba 28 yaani jana Jumamosi, watu wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki wameongoza shambulio la kinyama kwa wanaume na wanawake raia ambao walikuwa wakivuna mashamba yao huko Koshobe na jamii zingine za vijijini katika eneo la Serikali ya Mtaa wa Jere. 

Bwana Kallon ametuma salamu za rambirambi kwa familia za raia waliopoteza maisha katika shambulizi hili na akawatakia kupona haraka wale waliojeruhiwa.  

 “Tumepokea pia ripoti kwamba huenda wanawake kadhaa wametekwa nyara. Natoa wito wa kuachiliwa mara moja na kurudi katika usalama. Mawazo yangu pia ni pamoja na jamii za vijijini katika eneo hilo, ambao wameshtushwa na ukatili wa shambulio la jana na kuhofia usalama wao.” Amesema Bwana Kallon. 

Aidha Bwana Kallon ameeleza kuwa mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa na jamii ya kibinadamu inayofanya kazi ya kuokoa maisha na msaada wa maendeleo kwa walio hatarini zaidi katika Jimbo la Borno imekasirishwa na tukio hilo akieleza kuwa mashambulio hayo ya moja kwa moja dhidi ya raia wasio na hatia yanahatarisha uwezo wa watu walio katika mazingira magumu zaidi kunusurika shida zinazowakabili, na ambazo Umoja wa Mataifa unajitahidi kuzipunguza. 

Kallon ametoa wito akisema, “tukio hilo ni shambulio la moja kwa moja la vurugu dhidi ya raia wasio na hatia mwaka huu. Natoa wito kwa wahusika wa kitendo hiki kibaya na kisicho na maana wafikishwe mbele ya sheria. Kwa bahati mbaya ni mojawapo ya mashambulio mengi yanayowalenga wakulima, wavuvi na familia ambao wanajaribu kupata nafasi ya kutafuta riziki baada ya zaidi ya muongo mmoja wa mizozo. Ninalaani vikali shambulio hili na kitendo chochote cha unyanyasaji dhidi ya raia wasio na hatia na ninawasihi kabisa washiriki wote walio katika eneo kuheshimu sheria za kimataifa na ubinadamu.” 

Kiongozi huyo anayeuwakilisha Umoja wa Mataifa katika eneo hilo amesema wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia wako katika uhitaji mkubwa wa chakula na misaada mingine hususani katika kipindi hiki ambacho kuna viwango vikubwa vya njaa katika jimbo na Borno, na akaahidi kuwa Umoja wa Mataifa utajitahidi kadiri ya uwezo wake kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu.