Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni kwa vipi Rwanda imeweza kudhibiti COVID-19? 

Mwanamke akitembea kwenye kijiji cha Kageyo kilichoko mashariki mwa mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
WFP/Riccardo Gangale
Mwanamke akitembea kwenye kijiji cha Kageyo kilichoko mashariki mwa mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Ni kwa vipi Rwanda imeweza kudhibiti COVID-19? 

Afya

Uratibu wa kina wa serikali ya Rwanda ukiongozwa na ofisi ya Rais Paul Kagame na uzingatiaji wa mwongozo wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, (WHO) ndio msingi wa udhibiti wa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, (COVID-19) nchini Rwanda.

Rwanda inasema kuwa imekuwa ikichukua hatua za msingi ikiwemo kuchunguza ili kubaini wagonjwa, kufuatilia waambata wa wagonjwa wa coronavirus">COVID-19 na matumizi ya huduma za afya ya umma za kujikinga kama vile kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono. 

Waziri wa afya wa Rwanda Dkt. Daniel Ngamije amesema, “sera nzima ya kuzuia huu ugonjwa, ni kuanzia hatua za kujikinga, kama vile mtu kujikinga binafsi, kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono au kunawa mikono na kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu. Mikakati yote hii imetekelezwa na Wizara ya Afya kama ilivyopendekezwa na WHO, huku jamii nzima ikishiriki kuzuia COVID-19.” 

Akifafanua kuhusu msaada waliopata kutoka WHO, Dkt. Ngamije amesema, “WHO ilitusaidia kwa kutuanzisha mfumo thabiti wa ufuatiliaji. Baadhi ya wataalamu wao wa afya walikuwa sehemu ya timu yetu kuhakikisha kuwa tunaweza kuchunguza wagonjwa, kufuatilia waambata wao na kutoa ripoti sahihi kuhusu wagonjwa waliothibitishwa, wanaoshukiwa hadi pale itakapothibitika vinginevyo.” 

Uwepo pia kwa mifumo thabiti ya afya ya kuchukua hatua haraka imesaidia Rwanda kukabili COVID-19 ambapo Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha uchunguzi wa tiba Rwanda, Dkt, Sabin Nsanzimana anasema, “mikakati hiyo tofauti iliYOwekwa, baadhi ilikuwepo hata kabla ya kuwa na mgonjwa wa kwanza wa COVID-19. Tulianza mwaka mmoja uliopita. Tulikuwa na mlipuko wa Ebola kwenye ukanda wetu. Kwa hiyo tayari tulikuwa tumejiandaa kwa njia ambayo imetusaidia kujiandaa dhidi ya COVID-19.” 

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, tangu kupatikana kwa mgonjwa wa kwanza wa COVID-19 mwezi Machi mwaka huu hadi mwezi huu wa Novemba, Rwanda imekuwa na wagonjwa zaidi ya 4700 wa COVID-19 waliothibitishwa na kati yao hao 47 ndio waliofariki dunia.