Rwanda na Cote d’Ivoire miongoni mwa watakaonufaika na msaada wa chakula shuleni-WFP  

24 Novemba 2020

Wakati shule katika nchi zinazoendelea, zikianza kufunguliwa, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula, WFP limepokea msaada wa dola milioni 119 kutoka Idara ya kilimo ya serikali ya Marekani ili kusaidia kutoa chakula katika shule kwenye nchi za Asia na Afrika, imeeleza taarifa ya WFP iliyotolewa hii leo mjini Washington Marekani.  

Marekani hutoa ufadhili wa chakula cha shule kupitia mchakato wa tuzo ya ushindani inayosimamiwa kila mwaka na Mpango wa Chakula kwa ajili ya elimu wa Idara ya kilimo ya Marekani, USDA wa McGovern-Dole. 

Tuzo za sasa zinaifanya mipango ya WFP nchini Cote d'Ivoire, Laos, Nepal na Rwanda kupokea dola za Kimarekani milioni 25 kila moja, wakati mpango wa WFP nchini Bangladesh utapokea dola za Marekani milioni 19. 

Tuzo hizo, katika pesa taslimu na katika aina nyingine mbalimbali, zinaiwezesha WFP kulisha watoto wapatao 841,000 chini ya makubaliano ya miaka mitatu hadi mitano. Hii ni daraja muhimu kwa serikali za nchi hizi tano, kupewa msaada wa muda mpaka waweze kuanzisha mipango yao ya kudumu ya kutoa chakula shuleni.  

McGovern-Dole imekuwa ikitoa chakula shuleni katika katika nchi zinazoendelea tangu mwaka 2003, ikichangia kwa kiasi kikubwa ujifunzaji wa wanafunzi, afya na lishe. Kwa muda mrefu imekuwa moja ya vyanzo vikubwa vya fedha vya WFP kwa shughuli za kulisha shule, pamoja na mgao wa kupeleka nyumbani wakati shule zimefungwa kwa sababu ya COVID-19. Hadi sasa kwa mwaka huu, karibu watoto milioni 370 wamekosa chakula shuleni kwa mwaka huu, wakiwemo watoto milioni 13 wanaopokea chakula kutoka WFP.  

"Msaada huu bado ni ushahidi mwingine wa nguvu ya shughuli za kutoa chakula shuleni za WFP ulimwenguni na unakuja katika wakati mgumu." Anasema Carmen Burbano, Mkurugenzi wa mpnago wa chakula shuleni wa WFP akiwa Roma Italia.  

Programu za kutoa chakula shuleni za WFP zimeenea katika nchi 61 na msaada muhimu wa usalama wa jamii kwa kaya maskini na zilizo katika mazingira magumu. Katika mwaka 2019, WFP ilitoa chakula cha shule kwa watoto wa shule milioni 17.3, na kusaidia serikali mbalimbali kufikia watoto milioni 39 zaidi duniani. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter