Ukatili wa kingono na uhalifu wa kivita vyamsweka Sheka wa DRC jela maisha; MONUSCO yapongeza

23 Novemba 2020

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Leila Zerrougui, amekaribisha uamuzi wa mahakama ya kijeshi nchini humo wa kumpata na hatia na hatimaye kumhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela Ntabo Ntaberi Sheka.

Taarifa iliyotolewa leo huko Kinshasa mji mkuu wa DRC na ujumbe wa Umoja wa Mataiwa wa kuweka utulivu nchini humo, MONUSCO imesema Sheka alikuwa mkuu wa kikundi kilichojihami cha Nduma Defense of Congo, NDC ambapo hii leo yeye na washirika wake wamehukumiwa adhabu kwa makosa ya uhalifu wa kivita dhidi ya raia, hususan wanawake na watoto kati ya mwaka 2007 na 2017 wenye mji wa Walikale jimboni Kivu Kaskazini.

Uhalifu huo ni pamoja na uporaji, utumwa wa kingono, utumikishaji watoto vitani, uharibifu wa mali na vipigo kwa binadamu.

« Hukumu ya leo ni chanzo cha matumaini makubwa kwa manusura wa mzozo unaoendelea DRC. Machungu yamesikika na kutambulika, ukwepaji sheria hauwezekani tena. Hukumu pia inaashiria azma ya mamlaka za DRC za kuendelea, kupitia usaidizi wetu, vita vya kisheria dhidi ya wahalifu wote wa kivita DRC kwa siku zilizopita na sasa, » amesema Bi. Zerougui ambaye pia ni Mkuu wa MONUSCO.

Ntabo Ntaberi Sheka, kiongozi huyo wa zamani wa kikundi cha NDC kilichokuwa kinatekeleza uhalifu wake kwenye mji wa Walikale, alishtakiwa sambamba na washirika wake, Batechi Jean na  Lukambo Jean Claude aliyejulikana pia kama Kamutoto.

Mwingine ni Nzitonda Séraphin au  Lionso, kiongozi wa kikundi kilichojihami cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).

Katika hukumu hiyo Nzitonda Séraphin amehukumiwa kifungo cha maisha jela,  Lukambo Jean Claude kifungo cha miaka 15 jela ilhali Jean Batechi aliachiwa huru.

Kati ya julai 30 na Agosti 2 mwaka 2010, mashambulizi katika vijiji 13 huko Kibua-Mpofi yalisababisha vifo vya watu 287, huku watu wengine 380 wakiwemo wanawake, wanaume na watoto walikimbia makazi yao.

Kikundi hicho cha NDC pia kilitumikisha watoto 154 vitani ambapo ukiukwaji huo wa haki za binadamu ulirekodiwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud