Tuchukue hatua kukabili ajali za barabarani- Guterres

15 Novemba 2020

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kukumbuka waathirika wa ajali za barabarani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ajali za barabarani ni tatizo kubwa la kiafya na maendeleo ulimwenguni.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo, Guterres amesema kila siku watu 3,700 wakiwemo baba, mama, kaka, dada, watoto wa kike na wa kiume, marafiki na wafanyakazi hupoteza maisha yao kutokana na ajali za barabarani.

"Ajali za barabarani zinaongoza kwa vifo vya watoto wadogo na vijana wenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 29 na asilimia 90 ya ajali za barabarani hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati." Amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema hilo ni jambo linalopaswa kutiliwa maanani, "kama tunataka kuhakikisha tunakwamuka ipasavyo kutoka katika janga la Corona au COVID-19. Usalama lazima uwe kitovu cha mifumo yetu ya vyombo vya usafiri barabarani la sivyo hatutaweza kufikia lengo letu la kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya watu wanaofariki dunia kwa ajali za barabarani ifikapo mwaka 2030."

Guterres amekumbusha kuwa mikataba ya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani ni muhimu katika kusaidia nchi kushughulikia sababu kuu za ajali barabarani.

Amekaribisha azimio lililopitishwa hivi karibuni na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo baraza hilo limetangaza kipindi cha mwaka 2021 hadi 2030 kuwa ni muongo wa pili wa hatua kwa ajili ya usalama barabaranins kusihi kuungwa mkono kwa kazi za mjumbe maalum na mfuko maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani.

Na katika kuwakumbuka hii leo wale waliopoteza maisha kutokana na ajali za barabarani, Katibu Mkuu ametaka kila mtu aahidi kubuni mbinu mpya za kuhakikisha mifumo ya usafirishaji ni salama, ni rahisi kwa kila mtu na endelevu kwa kila mtu na kila pahali.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter