Hongera Wamarekani kwa kutekeleza haki ya demokrasia kwenye uchaguzi-UN
Hongera Wamarekani kwa kutekeleza haki ya demokrasia kwenye uchaguzi-UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewapongeza watu wa Marekani kwa kutekeleza demokrasia kupitia uchaguzi mkuu wa taifa hilo uliofanyika wiki iliyopita.
Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo Guterres amewapongeza Rais mteule na makamu wa Rais mteule kwa kuchaguliwa kwao katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 3.
Lakini pia amesisitiza kwamba ushirikiano baina ya Marekani na Umoja wa Mataifa ni nguzo muhimu katika ushirikiano wa kimataifa unaohitajika kushughulikia changamoto lukuki zinazoikabili dunia leo hii.
Pongezi zaidi kutoka UN
Salamu za hongera na pongezi kwa Rais mpya mteule wa Marekani Joe Biden na makamu wa Rais mpya mteule Kamala Harris zinaendelea kutolewa na viongozi mbalimbali wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kupitia kurasa zao za Twitter.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Audrey Azoulay ameandika” Hongera Rais mteule Joe Biden na makamu wa Rais mteule Kamala Harris. Changamoto za kimataifa leo hii zinahitaji ahadi na nguvu mpya kutoka Marekani kwa ajili manufaa ya pamoja katika sayansi, elimu, utamaduni. “
Pia amesema amefurahi kuona mwalimu Dkt. Biden kuingia ikulu ya Marekani White House.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women Phumzile Mlambo Ngucka naye ameandika “Hongera Rais mteule Joe Biden na makamu wa Rais mteule Kamala Harris. Kwa wanawake na wasichana kote duniani na hasa wanawake waliochanganya rangi huu ni wakati wa matumaini makubwa”
Ameongeza kuwa na kwa UN Women pia ni suala la kutia moyo hasa katika kizazi hiki cha usawa #GeberationEquality.
Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi hakusalia nyuma “ Pongezi sana Rais mteule Joe Biden na makamu wa Rais mteule Kamala Harris. Tuna matarajio makubwa ya kufanyakazi na uongozi wenu katika masuala ya kitaifa na kimataifa ya wakimbizi. Uongozi wa Marekani ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote kwa watu walio hatarini zaidi duniani.”
Naye mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM Antonio Vitorino amesema “Sote hapa IOM tunawapongeza Rais mteule Joe Biden na Makamu wa Rais mteule Kamala Harris tunarajia kufanyakazi na uongozi wenu katika kushughulikia suala la uhamiaji kwa faina ya wote.”