Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nalaani vikali shambulio la mjini Vienna Austria:Guterres 

Mji mkuu wa Austria, Vienna
Unsplash/Jacek Dylag
Mji mkuu wa Austria, Vienna

Nalaani vikali shambulio la mjini Vienna Austria:Guterres 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulio la kikatili lililofanyika mjini Vienna Austria na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine kadhaa. 

Kwa mujibu wa duru za Habari mtu wenye silaha alifyatua risasi Jumatatu jioni saa za Vienna katikati yam ji huo katika maeneo tofauti. Mtu mmoja alifariki katika eneo la tukio wakati mtu wa pili alifariki dunia baadaye kutokana na majeraha aliyopata.  

Watu wengine 14 walijeruhiwa na baadhi yao vibaya sana hivi sasa wako hospitali wanatibiwa. 

Miongoni mwa watu waliojeruhiwa ni askari wa usalama. 

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema anafuatilia kwa hofu hali hiyo mjini Vienna na amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa kwa watu bna serikali ya Austria. 

Bwana. Guterres pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia ahuweni ya haraka majeruhi. 

Mshikamano na waathirika 

Mji wa Vienna ni mwenyeji wa ofisi muhimu za Umoja wa Mataifa ambazo ni Pamoja na makao makuu ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC, shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA na shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO. 

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter mkurugenzi mtendaji wa UNODC, Ghada Wally ambaye pia ndiye mkurugenzi mkuu wa ofisi ya Vienna (UNOV) ameto apole pia kwa waathirika wa shambulio hilo. 

“Mawazo na pole zangu zinakwenda kwa wahanga na wale wote walioathirika na shambulio hili la kikatili mjini kwetu. Jumuiya ya Umoja wa Mataifa mjini Vienna inasimama Pamoja na watu wa Austria katika wakati huu mgumu.” 

Mshangao na kutoamini 

Na katika taarifa iliyotolewa mapema leo mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya muungano wa ustaarabu UNAOC, Miguel Angel Moratinos ameelezea kushtushwa na kushangazwa na shambulio hilo la katikati yam ji wa Vienna. 

Mwakilishihuyo anayehusika na masuala ya kuchagiza kuvumiliana katika masuala ya kidini na kulinda maeneo ya kidini amelaani pia shambulio hilo na kusisitiza kwamba “vitendo hivyo vya kigaidi havivumiliki na hakuna kinachovihalalisha popote, wakatoi wote na kwa yeyote anayevitekeleza.”