Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani vikali shambulio kwenye kituo cha treni cha Kramatorsk Ukraine

Lyuba akiwa na mwanae wa miezi miwili akiwa kwenye kituo cha reli Uzhhorod baada ya kukimbia mzozo.
© UNICEF/Olena Hrom
Lyuba akiwa na mwanae wa miezi miwili akiwa kwenye kituo cha reli Uzhhorod baada ya kukimbia mzozo.

UN yalaani vikali shambulio kwenye kituo cha treni cha Kramatorsk Ukraine

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa leo umelaani vikali shambulio lililotekea kwenye stesheni ya treni ya Kramatorsk Kaskazini mwa jimbo la Donetsk nchini Ukraine linalodaiwa kukatili maisha ya raia 39 miongoni mwao ni watoto na kujeruhi wengine wengi waliwemo waliojeruhiwa vibaya sana.

Katika ujumbe wake wa kulaani vikali shambulio hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Shambulio hilo kwenye  kituo cha reli cha hii leo, ambalo limesababisha vifo na kujeruhi raia wengi waliokuwa wakisubiri kuhamishwa, wakiwemo wanawake wengi, watoto na wazee, na mashambulizi mengine dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, hayakubaliki kabisa. Ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu, ambazo wahusika lazima wawajibishwe.” 

Amezikumbusha pande zote katika mzozo wajibu wao chini ya sheria za kimataifa wa kulinda raia na udharura wa kukubaliana juu ya usitishaji mapigano wa kibinadamu ili kuwezesha uokoaji salama na ufikiaji muhimu wa misaada kwa watu walionaswa katika migogoro.  

Katibu Mkuu anasisitiza wito wake kwa wote wanaohusika kukomesha mara moja vita hivi vya kikatili. 

Idadi ya vifo huenda ikaongezeka 

Kwa upande wake Mratibu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mgogoro wa Ukraine, Amin Awad, amesema kuwa wengi wamejeruhiwa vibaya na kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka. 

Ameongeza kuwa "Imeripotiwa sana katika siku mbili zilizopita kwamba kituo na eneo jirani lilikuwa limejaa raia wanaojaribu kukimbia uhasama unaozidi kuenea nchini humo. Tumesikitishwa sana na ripoti za watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu watu walio hatarini zaidi katika eneo la Kramatorsk ambao wamekumbwa katika shambulio hili." 

Bwana Awad amesema matumizi ya silaha za milipuko, "yenye athari kubwa katika maeneo yenye wakazi wengi ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Vikosi vyote vya kijeshi, katika migogoro yote, havipaswi kufanya mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia. Lazima wafanye kilka liwezekanalo ili kulinda raia." 

Aliongeza kuwa hospitali katika maeneo jirani sasa zimejaa majeruhi: "Sisi na washirika wetu wa kibinadamu tuko tayari kufanya chochote tunachoweza kusaidia wale ambao wanajibu mashambulizi na wale walionusurika. Tumepeleka vifaa vya huduma ya kwanza pia. kama mgao wa dharura wa chakula, tembe za kusafisha maji na mablanketi." 

Amesisitiza kuwa "Tunaendelea kutoa wito kwa wahusika wote katika mzozo huu kuruhusu kupita kwa usalama na bila vikwazo kwa watu wanaotaka kuondoka, kuzuia mashambulizi ya usafiri muhimu kwa raia, na misaada ya kuokoa maisha kufikia wale ambao hawawezi kusonga au kuondoka. " 

Wakimbizi kutoka Ukraine wakisubiri kujiandikisha kwa ajili ya msaada wa pesa taslimu Warsaw, Poland.
© UNHCR/Maciej Moskwa
Wakimbizi kutoka Ukraine wakisubiri kujiandikisha kwa ajili ya msaada wa pesa taslimu Warsaw, Poland.

Hitaji la dharura la usitishaji mapigano 

Usitishaji mapigano wa ndani unahitajika kwa dharura zaidi kuliko hapo awali nchini Ukraine huku mzozo ukielekea katika maeneo ya mashariki kufuatia Urusi kujiondoa katika eneo karibu na mji mkuu Kyiv, wahisani wa Umoja wa Mataifa walisema, huku bei za vyakula duniani zikipanda na kufikia viwango vya juu zaidi. 

Wiki sita tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi, maelfu ya raia wanaaminika kuwa bado wamenaswa katika bandari ya kusini mwa mji wa Mariupol, ambapo wamekabiliwa na wiki za kuvurumishwa makombora mazito. 

Lakini bado hakuna makubaliano ya mapatano kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine kuwaacha watu watoroke salama, huku kukiwa na juhudi za upatanishi zinazofanywa na mkuu wa Umoja wa Mataifa wa shirika la kutoa misaada ya dharura OCHA Martin Griffiths. 

Hofu yetu kubwa ni watoto: UNICEF 

Naye mwakilishi wa shirika la Umoja wa matifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Ukraine Murat Sahin amesema "Tunalaani vikali shambulio la leo kwenye kituo cha treni huko Kramatorsk, Ukraine. Hatujui bado ni watoto wangapi waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo, lakini tunahofia shambulio hilo ni baya zaidi. Kituo cha treni cha Kramatorsk kimekuwa njia kuu ya maelfu kwa maelfu ya watu na familia zinazohama kutoka eneo la Donetsk, ambalo limeshuhudia uharibifu mbaya zaidi wa vita, kwenda kwenye maeneo salama zaidi nchini Ukraine.” 

Ameongeza kuwa “Mapema leo, UNICEF ilishusha vifaa vya matibabu na vifaa vya dharura huko Kramatorsk. Wiki iliyopita, UNICEF imewasilisha takriban tani 50 za vifaa vya kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na dawa, maji na vifaa vya usafi huko Kramatorsk ili kukabiliana na hali ya kibinadamu inayozidi kuzorota kwa kasi mashariki. Timu ya UNICEF ilikuwa ikipeleka vifaa vya kuokoa maisha kwa idara ya afya ya mkoa, kilomita moja kutoka kituo cha treni wakati shambulio hilo lilipotokea. Rais na hususan watoto lazima walindwe dhidi ya mashambulizi. Mauaji ya watoto lazima yakome sasa.”