Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Côte d’Ivoire chunguzeni kwa kina na bila upendelezo mauaji ya watu 20- OHCHR

Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu.
Photo UN Multimedia
Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu.

Côte d’Ivoire chunguzeni kwa kina na bila upendelezo mauaji ya watu 20- OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesihi serikali ya Cote d’Ivoire ihakikishe uwajibikaji kwa watu wanaohusika na mauaji ya watu 20 yaliyotokea baada ya mapigano ya kikabila na majibizano kati ya polisi na wafuasi wa vkundi vya upinzani nchini huo kwenye vitongoji mbalimbali nchini humo.

Matukio hayo yameripotiwa wakati huu ambapo taifa hilo la Afrika Magharibi linajiandaa kwa uchaguzi mkuu tarehe 31 mwezi huu wa Oktoba.

Msemaji wa OHCHR, Ravina Shamdasani akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswsi hii leo amesema, "mapigano ya kikabila yameripotiwa katika miji ya Bongouanou kusini mwa taifa hilo na Dabou kusini-mashariki kati ya tarehe 17 na 21 mwezi huu wa Oktoba. Katika maeneo mengine ya mji mkuu wa kibiashara, Abidjan, watu wasiofahamka walishambulia na kutishia waandamanaji kwa kutumia mapanga na visu huku wakiwepa sheria. Katika baadhi ya matukio, vituo vya kupigia kura vimeharibiwa, kadi za watu za kupigia kura halikadhalika huku maeneo ya kibiashara yakiporwa."

Bi.Shamdasani amesema ili kuzuia kutokea tena kwa vitendo kama hivyo, ni muhimu kwa mamlaka kufanya uchungzi wa haraka, wa kina na huru dhidi ya matukio yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu bila kujadli mrengo wa kisiasa wa washukiwa wa matukio hayo.

Amesema wanatambua kuwa watu kadhaa wanashikiliwa kuhusiana na ghasia huko Dabou.

Kauli za chuki nazo zimeshamiri, ukabila wageuzwa mtaji wa kisiasa

Amesema pia wana hofu kubwa kutokana na kuendelea kwa matumizi ya lugha za chuki na chochezi ambazo amesema zinaongeza ubaguzi na ghasia dhidi ya makabila na wafuasi wa vyama vya siasa, akifafanua kuwa lugha hizo zinatumika majukwaani na pia kwenye mitandao.

Msemaji huyo wa OHCHR amesema kwa kuzingatia "historia ya ghasia zihusianazo na uchaguzi Côte d’Ivoire, tunasihi vyama vyote vijizuie kutumia lugha za kibaguzi na chochezi kwa misingi ya kikabila na vyama kwa kuwa zitazidi kuongeza mgawanyiko kwenye jamii na kisha ghasia."

Ametoa wito kwa mamlaka kulinda haki za ushiriki kisiasa kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kuhakikisha kuwa watu wanatekeleza wajibu wao bila ubaguzi, hofu wala kulipiziwa kisasi.

Ametamatisha akisema kuwa mamlaka zihakikishe kuheshimiwa kwa haki za mikusanyiko kwa amani na zikinge mashambulizi kutoka pande za tatu na kwamba "tunaomba utulivu kuelekea uchaguzi na hata baada ya uchaguzi na iwapo kuna tofauti zozote basi zisuluhishwe kwa njia ya mazungumzo."