Licha ya hatua kuchukuliwa, bado maelfu Côte d’Ivoire  hawana utaifa

Kama ilivyo kwa wahamiaji nchini Ivory Coast, pia warohingya ambao ni kabila kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar, hawana uraia na hawana utambulisho wowote. Hapa ni Cox's Bazar nchini Bangladesh wakiwa hawajui hatma ya kurejea nchini mwao.
K M Asad/UN
Kama ilivyo kwa wahamiaji nchini Ivory Coast, pia warohingya ambao ni kabila kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar, hawana uraia na hawana utambulisho wowote. Hapa ni Cox's Bazar nchini Bangladesh wakiwa hawajui hatma ya kurejea nchini mwao.

Licha ya hatua kuchukuliwa, bado maelfu Côte d’Ivoire  hawana utaifa

Haki za binadamu

Nchini Côte d’Ivoire  maelfu ya watu waliohamia nchini  humo wanasubiri mwelekeo mpya utakaowawezesha kupata utaifa na hivyo kunufaika na huduma za kiuchumi na kijamii. Jason Nyakundi na taarifa kamili.

Miongoni mwa maelfu ya wahamiaji hao wasio na utaifa ni Aminata Sidibé ambaye alizaliwa nchini Côte d’Ivoire mwaka 1960, taifa hilo lilipopata uhuru. Vizazi vitatu vya familia yake vimefuatia baada yake lakini wote tatizo lao hawatambuliwi kuwa raia wa nchi hiyo, vikwazo vya kisheria ndio tatizo.

Aminata na familia yake ni jamii ya Fula ambao ni wafugaji wa kuhamahama, wakipatikana katika mataifa 10 ya Afrika Magharibi na Kati,  “Mungu aliona wazazi wangu walikuja hapa. Nimezaliwa hapa, walifia hapa na kuniacha mimi hapa. Niliolewa, nimepata watoto na watoto wa watoto wangu. Iwapo watu wanasema mimi si wa hapa, je mimi niseme nini?”

Mamilioni ya watu duniani hawana utaifa na hivyo wanakosa haki zao za msingi kama elimu, afya, ajira na uhuru wa kutembea.

Aminata na familia yake ni wafugaji lakini hawawezi kumiliki ardhi, haki za kulisha mifugo ni makubaliano yao na mmiliki wa ardhi n ahata hawawezi kuomba mkopo benki au kupata leseni ya udereva.

Nchini Côte d'Ivoire maamuzi matatu ya kihistoria yaliwezesha watoto 11 waliokuwa wametelekezwa nchini humo kupatiwa uraia lakini bado Aminata na maelfu wengine hawajui hatma yao.

Sheria mpya iliyoanzisha kanuni mahsusi ya kuruhusu kupata cheti cha kuzaliwa baada ya kuchelewa kuwasilisha itasaidia mamia ya maelfu kupata haki ya utaifa kama anavyosema Seydou Tall.

“Tunataka watoto wetu wapate  nyaraka ili waweze kusoma zaidi. Hii ni muhimu sana kwetu.”

Mwaka 2018 Côte d’Ivoire kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR ilifanya tathmini ya hali halisi ya idadi ya watu wasio na utaifa na hadi sasa takwimu bado hazijatolewa.

Mwezi Mei mwaka 2017, Afrika Magharibi ilikuwa ukanda wa kwanza kuandaa mpango wa utekelezaji wa kikanda wa Banjul wenye nguvu kwa lengo la kutokomeza ukosefu wa utaifa miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.