Harakati za UNHCR nchini Côte d’Ivoire zanusuru watoto wasiokuwa na utaifa

10 Aprili 2019

Nchini Côte d’Ivoire, kampeni kabambe iliyoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na watetezi wa haki kuhusu haki ya mtu kupata utaifa imezaa matundana kuleta nuru kwa wasichana wawili ambao tangu kuzaliwa hadi kutimiza umri wa miaka 17 nchini humo hawakuwa na utaifa.

Wasichana hao Christelle Karidja Camara na Françoise Yeo Pandjawa ambao mama zao walifariki dunia punde tu baada ya kujifungua wameishi pamoja kwenye kituo cha watoto yatima cha KORHOGO nchini Côte d’Ivoire baada ya baba zao kukataa kuwatambua na hivyo hawakuweza kutambuliwa.

Kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo, ili kupata kitambulisho cha uraia au cheti cha kuzaliwa ni lazima kuthibitisha kuwa mzazi mmoja ni mzawa wa Côte d’Ivoire.

Katika kituo cha watoto yatima, Christelle na Françoise wanalea watoto wengine wadogo wa kike na wa kiume kwa kuhakikisha wanawaogesha, wanawalisha, wanawapeleka shule na pia kucheza nao.

Mlezi wao, Michel ambaye naye amekulia kwenye kituo cha watoto yatima, hana pia utaifa na anasema,  “nchini Côte d’Ivoire angalau mzazi mmoja awe mzawa. Iwapo huwezi kuthibitisha utaifa wa angalau mzazi mmoja, unakuwa huna utaifa, hata kama una asili ya taifa hili. Inakatisha tamaa.”

Uamuzi wa mwaka jana wa mahakama ulikuwa ndio jawabu sahihi kwa Christelle na Françoise ambapo hivi karibuni wamepokea nyaraka muhimu zinazothibitisha utaifa wao kama ambavyo Layse Farias, Afisa ulinzi wa UNHCR anasema kuwa, “hii inaweka mazingira ya utambulisho wa kisheria kwa watoto hawa. Sasa wanaweza kufanya tukio lolote la kiraia kwenye maisha yao ikiwemo ndoa, kumaliza masomo yao hadi Chuo Kikuu na kupata ajira rasmi. Si hivyo tu, kwa wao inamaanisha pia kujumuishwa kwenye  taifa.”

Mwezi Mei mwaka 2017, Afrika Magharibi ilikuwa ukanda wa kwanza kuandaa mpango wa utekelezaji wa kikanda wa Banjul wenye nguvu kwa lengo la kutokomeza ukosefu wa utaifa miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.

Ikiwa imesalia miaka 6 kutokomeza ukosefu wa utaifa, hatua kubwa zimepigwa mathalani Côte d’Ivoire, ikiwemo kwa watoto waliotelekezwa na wasio na uwezo wa kubainisha familia zao kama ilivyokuwa kwa Françoise na Christelle, ambapo  uamuzi wa mahakama mwezi Oktoba mwaka 2018 uliwezesha wao na wenzao 9 kupata uraia.

Halikadhalika  Côte d’Ivoire imepitisha sheria mpya yenye kanuni mahsusi kwa ajili ya wale waliochelewa kusajili uzazi, kuandaa upya nyaraka za utambulisho na nyaraka za uzazi, hatua ambazo zitasaidia mamia ya maelfu ya watu walio hatarini kukosa utaifa nchini humo.

Kwa sasa UNHCR inashirikiana na shirika la kiraia nchini humo kuchagiza kampeni za marekebisho ya kisheria na mabadiliko ya kanuni za utawala ili kusaidia walio hatarini kukosa utaifa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud