Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadau waandaa mkutano wa kuchangisha fedha kusaidia warohingya

Maelfu ya wakimbizi wa Rohingya wanaishi katika kambi ya Hakimpara iliyopo Cox's Bazar, Bangladesh
OCHA/Vincent Tremeau
Maelfu ya wakimbizi wa Rohingya wanaishi katika kambi ya Hakimpara iliyopo Cox's Bazar, Bangladesh

Wadau waandaa mkutano wa kuchangisha fedha kusaidia warohingya

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati kunafanyika mkutano wa wahisani ili kusaidia wakimbizi wa kabila la Rohingya nchini Myanmar ambao wengine wamekimbilia nchi jirani ikiwemo Bangladesh, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linasisitiza umuhimu wa usaidizi wa kimataifa na kuongeza maradufu jitihada za kusaka suluhu kwa jamii ambayo haina utaifa na imekimbia makwao.

Taarifa iliyotolewa awali na UNHCR imesema msaada wa huduma muhimu katika jamii wenyeji ni muhimu pia na usaidizi unaoendelea hivi sasa unakabiliwa na upungufu mkubwa katika mwaka huu kwa kuwa kiasi cha fedha kilichoombwa ni chini ya nusu yake ndiyo imeshapokelewa hadi sasa. Katika mwaka huu wa 2020, Umoja wa Mataifa umeomba zaidi ya dola bilioni 1 za kimarekani ili kufikia mahitaji ya kibinadamu ya wakimbizi wa Rohingya walioko Bangladesh. Kusambaa kwa janga la COVID-19 kumepigilia msumari wa moto kwenye kidonda.   

Hivi sasa wakimbizi wa Rohingya 860,000 wanaishi katika makazi kote katika wilaya ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh. Wengi wa wakimbizi hao, kama 740,000, walikimbia kutoka Myanmar wakati wa mgogoro wa hivi karibuni mwaka 2017.Nchi nyingine katika ukanda huo zinawahifadhi takribani wakimbizi wa Rohingya 150,000 huku ikikadiriwa kuwa takribani wakimbizi 600,000 wanaishi katika jimbo la Rakhnine nchini Myanmar.  

Katika eneo lote, Warohingya wengi wanaishi pembezoni na wanahitaji kuhakikishiwa upatikanaji wa huduma za msingi za afya, maji safi na salama ya kunywa, chakula cha kuaminika, au kazi ya maana na fursa za elimu. Janga la COVID-19 limedhoofisha hali zao za maisha, kufanya upatikanaji wa huduma kuwa changamoto zaidi, kuongezeka kwa hatari ya unyanyasaji wa kingono na kijinsia, na kuzidisha athari za magonjwa ya kuambukiza kwa Rohingya waliokimbia makazi yao wanaoishi katika kambi zenye watu wengi, kama vile zile za Cox’s Bazar na katika Jimbo la Rakhine. 

Mtoto akiwa amebeba maji huko Cox's Bazar nchini Bangladesh (10 Julai 2019)
© UNICEF Patrick Brown
Mtoto akiwa amebeba maji huko Cox's Bazar nchini Bangladesh (10 Julai 2019)

 

UNHCR inasisitiza kuwa jamii ya kimataifa na nchi katika eneo hazipaswi tu kudumisha msaada kwa wakimbizi na wenyeji wao, lakini pia kubadilika kulingana na mahitaji mapya muhimu na kupanua utaftaji wa suluhisho. 

“Utafutaji wa suluhishisho la mgogoro ulenge katika watu kurejea kwa hiyari, salama na endelevu kwa wakimbizi wa Rohingya katika maeneo yao au kwingine watakakochagua katika Myanmar.” Inashauri UNHCR 

Aidha UNHCR imesema jukumu la kuunda mazingira yanayofaa kurudi salama na endelevu ya wakimbizi wa Rohingya liko kwa mamlaka ya Myanmar. Utaratibu huu utahitaji kushirikisha jamii nzima, kufungua na kuongeza mazungumzo kati ya mamlaka ya Myanmar na wakimbizi wa Rohingya na kuchukua hatua zinazosaidia kujenga ujasiri na uaminifu. Hii ni pamoja na kuondoa vizuizi kwa uhuru wa kusafiri, kuwezesha warohingya waliofurushwa kurejea vijijini mwao na kuwapatia njia ya wazi ya uraia.