Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila udhibiti mzuri wa hatari ya majanga, hali mbaya huzidi kuwa mbaya zaidi-Guterres  

Kimbunga Matthew kilipoitikisa Haiti
UN/Logan Abassi
Kimbunga Matthew kilipoitikisa Haiti

Bila udhibiti mzuri wa hatari ya majanga, hali mbaya huzidi kuwa mbaya zaidi-Guterres  

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupunguza hatari ya majanga, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuwa janga la COVID-19 limeleta umakini mpya kuhusu umuhimu wa kuimarisha upunguzaji wa hatari za majanga kwani hali mbaya zinazidi kuwa mbaya zaidi pindi panapokosekana udhibiti mzuri wa hatari za majanga.

Akizungumza kwa njia ya video kuhusu siku hii ambayo ilianza mnamo mwaka 1989 baada ya wito wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  ili kukuza utamaduni wa ulimwengu wa uelewa wa hatari na upunguzaji majanga, Bwana Guterres amesema  nchi nyingi zinakabiliana na majanga mengi mfululizo,  matukio makubwa ya hali ya hewa yameongezeka sana katika miongo miwili iliyopita ingawa kumeshuhudiwa maendeleo madogo kuhusu kupunguza uharibifu wa mabadiliko ya tabianchi na mazingira.  

“Hatari ya majanga sio jukumu la mamlaka za mitaa na kitaifa pekee. COVID-19 imetuonesha kuwa hatari ya kimfumo inahitaji ushirikiano wa kimataifa. Udhibiti mzuri wa hatari ya majanga unamaanisha kuchukua hatua kwa sayansi na ushahidi.” 

Ili kutokomeza umaskini na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, lazima tuweke umma juu ya mambo mengine yote. 

"Kwa sababu hizi na zaidi, Siku ya Kimataifa ya mwaka huu ya kupunguza hatari ya majanga inahusu kuimarisha udhibiti wa hatari za majanga ili kujenga ulimwengu salama na wenye mnepo zaidi." 

 Awali, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya majanga, UNDRR Mami Mizutori naye alikuwa amekumbusha kuwa usimamizi bora wa majanga unategemea uongozi wa kisiasa na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kupitia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na mkataba wa Sendai wa kupunguza athari za majanga uliopitishwa miaka mitano iliyopita.