Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imetupatia fursa ya kuchagua mwenendo tuutakao – Papa Francis

Papa Francis (kwenye skrini) ambaye ndiye kiongozi wa Holy See akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 kutoka Vatican.
UN/ Evans schneider
Papa Francis (kwenye skrini) ambaye ndiye kiongozi wa Holy See akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 kutoka Vatican.

COVID-19 imetupatia fursa ya kuchagua mwenendo tuutakao – Papa Francis

Afya

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukiwa umeingia siku ya nne hii leo, Holy See ambayo ni mjumbe  au Observer, kwenye Umoja wa Mataifai imehutubia wajumbe kwa njia video, kama ilivyo ada katika mkutano huu unaofanyika huku janga la Corona au COVID-19 likiwa linaendelea kugubika baadhi ya maeneo duniani ikiwemo Marekani.

 

Akisoma hotuba yake kutoka Vatican, Mkuu wa kanisa katoliki dunia ambaye ndiye kiongozi wa Holy See, Papa Francis, amesema janga la Corona “penginepo ni njia ya sisi kufikiria upya mienendo yetu ya maisha na mifumo yetu ya uchumi na kijamii ambayo inazidi kuongeza pengo kati ya maskini na tajiri.”

Papa Francis amesema janga la Corona, linataka dunia itumie fursa hii ya majaribu kama wakati wa kuchagua, “wakati wa kuchagua kile ambacho ni muhimu na kile ambacho hakina umuhimu wowote, wakati wa kutenganisha kati ya kipi ni mahitaji na kipi si hitaji muhimu.”

Amefafanua kuwa, kuna mwenendo unasisitiza kujitosheleza, utaifa, kuzuia ushirikiano na nchi, ubinafsi na kujitenga, njia ambazo amesema zinaengua maskini, wale walio hatarini na wale wanaoishi pembezoni.

Amesema kuwa bila shaka mwenendo huo utakuwa na madhara kwa jamii nzima, na kujisababishia majeraha akisema kuwa katu mwenendo huu hautakiwi.

Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki amesema janga la sasa ni fursa kwa Umoja wa Mataifa kusaidia kujenga jamii yenye udugu zaidi na upendo. “Hii inajumuisha kuzingatia upya dhima ya taasisi za uchumi na fedha, taasisi kama vile Benki ya Dunia na shirika la fedha duniani, IMF, ambazo zinapaswa kushughulikia mapema pengo linaloongezeka kati ya nchi tajiri zaidi na zile zilizotwama kwenye lindi la umaskini.”

Hotuba ya Papa Francis kwa njia ya video ilikuwa imerekodiwa mapema na kurushwa kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati huu wa janga la COVID-19ambalo limezuia viongozi kushiriki wao wenyewe ukumbini.

Badala yake, wawakilishi wa nchi wanachama wanakuwepo ukumbini na kukaribisha hotuba hizo kabla ya mkanda wa video kuchezwa.

Hii ni mara ya kwanza kwa mjadala mkuu wa UNGA kufanyika mtandaoni na ukumbini.