Mtaalam huru wa UN akaribisha uamuzi wa Papa Francis wa kuondoa pazia la siri kuhusu ukatili dhidi ya watoto

19 Disemba 2019

Ni lazima Vatican ichukue hatua kuhakikisha haki kwa watu ambao walinyanyaswa kingono na watawa walipokuwa watoto amesema mtaalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Alhamisi.

Maud de Boer-Buquicchio, mtaalam huru kuhusu biashara haramu ya binadamu na utumikishwaji wa watoto amesema hayo kupitia tarifa ya kukaribisha uamuzi wa Papa Francis wa kuondoa sera ya kanisa la katoliki ya kuweka siri ya visa vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto.

Mtaalam huyo huru amesema, “pazia la siri ambalo lilikuwa linazingira uhalifu huo na ambalo lilizuia wahanga kupata haki na marekebisho limeraruliwa

Hatahivyo, kuondolewa kwa sera hiyo ya siri ni hatua ya kwanza kwa mujibu wa Bi. Boer-Buquicchio ambaye ameongeza kuwa, “Vatican inahitaji kuchukua hatua muhimu kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa wahanga kote ulimwenguni na inafanyika kupitia uchunguzi wa haraka na wa kina na ambao uko wazi kwa umma, kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya washukiwa na kuhakikisha utoaji ripoti kwa wafanyakazi wa kanisa walio na tarifa kuhusu vitendo hivyo vya uhalifu.”

Amesisitiza kwamba kanisa linahitaji kuanzisha sera ya kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto katika taasisi zote chini yake na kuhakikisha kufukuzwa mara moja wale wanaopatikana kutekeleza ukatili huo dhidi ya watoto.

Bi. de Boer-Buquicchio amekumbusha kwamba awali ukatili huo, “ulikuwa unapuuzwa, kukanwa au kutajwa kama dhambi ambayo inaweza kutatuliwa iwapo mtu ataomba radhi na kutubu.”

Amesema kwamba wahanga wote wanahitaji kufidiwa pamoja na kupokea matibabu kwa kuzingatia madhila waliyoyapitia, na kwamba kanisa linahitaji kwa haraka kuwapa msaada wa kupata ushauri na msaada wa kijamii.

Halikadhalika ametoa wito kwa serikali kutimiza wajibu wao ikiwemo kulinda watoto dhidi ya aina hizo za ukatili akiongeza, “tunashukuru wahanga kwa ujasiri wao wa kuzungumza kuhusu swala hili, lakini mzigo wa kutatua uhalifu huu sio wao tu. Dunia inasubiri mataifa na kanisa kuchukua jukumu lake na kutokomeza vitendo hivyo. Vitendo vinahitaji kuja baada ya maneno.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter