Vyombo vya habari vilichangia hofu miongoni mwa wananchi Brazil kuhusu COVID-19

22 Septemba 2020

Rais wa Brazil,  Jair Bolsorano akiwa wa kwanza kuzungumza amesema ni heshima kubwa kwake kuhutubia nchi zilizo huru wakati ambapo dunia inahitaji ukweli ili kukabili changamoto. 

Amesema COVID-19 imekuwa jambo linalotikisa ulimwengu kwa mwaka huu wote, “na nitume salamu zangu za rambirambi kwa familia za wote waliopoteza maisha.” 

Rais Bolsonaro amesema kwa nchi  yake yeye, “mwanzoni kabisa nilionya kuwa tuna matatizo mawili ya kutatua; COVID-19 na ukosefu wa ajira na kwamba matatizo yote hayo mawili yanapaswa kushughulikiwa pamoja kwa kiwango sawia cha uwajibikaji. Hatua zote za kutochangamana zilizizngatiwa katika majimbo yote 27.” 

Amesema kuwa serikali ilisambaza rasilimali zote zinazotakiwa ili kukabili virusi hivyo lakini akatupia lawama baadhi ya vyombo vya habari vya Brazil kwa kuingiza masuala ya siasa kwenye janga la COVID-19, “kwa kujenga hofu miongoni mwa jamii kwa kutaka wananchi wake nyumbani na kisha suala la uchumi lishughulikiwe baadaye. Jambo hili lilileta ghasia nchini.  

Hata hivyo amesema serikali ilikuwa jasiri na kusambaza misaada ikiwemo takribani dola 1,000 kwa familia milioni 65 maskini nchini Brazil sambamba na msaada kwa familia za watu wa jamii ya asili. 

Kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, duniani kote idadi ya wagonjwa wa COVID-19 waliothibitishwa ni 4,544,629 ambapo kwa waliofariki dunia Brazil ni 136,895 tangu kuanza kwa janga hilo.

Rais Bolsonaro amesema kuwa janga la Corona limekuwa fundisho kubwa kwamba, “hatuwezi kutegemea tu mataifa machache katika kutengeneza vifaa muhimu ambavyo ni muhimu kwa uhai wetu.”

Ekari kadhaa za msitu wa Amazon zimetiwa moto ili kupitisha mashamba ya miwa na maharagwe ya soya bila kujali madhara kwa mazingira.
UNEP GRID Arendal/Riccardo Pravettoni
Ekari kadhaa za msitu wa Amazon zimetiwa moto ili kupitisha mashamba ya miwa na maharagwe ya soya bila kujali madhara kwa mazingira.

Kuhusu mazingira, Rais huyo wa Brazil amesema kuwa taifa lake ni moja ya mataifa  yanayoongoza duniani kwa uzalishaji wa chakula n ani kwa sababu hiyo, kuna mvuto mwingi wa kueneza taarifa potofu kuhusu mazingira nchini humo.

“Msitu wetu wa kitropiki ni kwa mantiki hiyo hauwezi kuruhusu kusambaa kwa moto. Milipuko ya moto inaonekana kuwepo eneo moja tu mashariki mwa msitu, ambako raia wa Brazili wa jamii ya asili wanachoma maeneo yao ya mashamba wakijisakia kipato katika maeneo ambayo tayari yameshakatwa miti. Moto ambao unawashwa kwa sababu za kihalifu tunapambana nao kwa nguvu zote,” amesema Rais Bolsonaro.

Kwa mujibu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, mioto ya misituni nchini Brazil imekuwa ikiwashwa makusudi ili kufanikisha upanzi wa mashamba ya michikikichi na maharagwe aina ya soya au kwa ajili ya malisho ya mifugo.
 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter