Tuimarishe mshikamano vita dhidi ya COVID-19 na tukomeshe hewa ukaa ifikapo 2060: China 

22 Septemba 2020

Rais wa Uchina Xi Jinping ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa kupambana na virusi vya corona wakati wa hotuba yake hii leo kwenye mjadala wa Baraza Kuu akidai kwamba nchi yake inalenga kuwa huru bila hewa ukaa katika vita kubwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2060. 

“Tunapaswa kufuata muongozo wa kisayansi, kuzingatia na kufuata maagizo na jukumu la shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na kuanzisha hatua za kimataifa kupambana na janga la COVID-19.” 

Kabla ya kuchezwa hotuba yake iliyorekodiwa kwa njia ya video kwenye ukumbi wa Baraza Kuu , alitambulishwa na balozi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Zhang Jun, ambaye bila kutaja moja kwa moja Marekani amejibu wito uliotolewa hapo kabla na Rais wa Marekani Donald Trump wa kutaka China kuwajibishwa kwa kusambaza virusi vya corona. 

Balozi Jun amesema, “Uchina inapinga vikali shutuma zisizo na msingi wowote dhidi yake. Ubinadamu utashinda katika vita hivi dhidi ya corona.”. 

Rais Jinping amezungumzia dhidi ya kusontana vidole akisistiza kwamba, “jaribio lolote la kulifanya suala la COVID-19 kuwa la kisiasa ya unyanyapaa lazima likataliwe.” 

Sote ni familia moja 

Rais huyo wa Uchina ameisihi dunia kutambua kwamba, “tunapaswa kuona kuwa sote ni watu wa familia moja kubwa, tusake ushirikiano wa faida kwa wote na kuweka maslahi ya jumla mbele ya dhana ya migogoro, na la msingi zaidi tunapaswa kuheshimu chaguo la nchi huru la njia na muundo wa maendeleo.” 

Amesema dunia haipaswi kukwepa changamoto za kimataifa za uchumi, uchumi ulio wazi na kuzingatia ushirikiano wa kimataifa wa biashara na kulifanya shirika la biashara duniani WTO kama nguzo katika hili. 

Akizungumzia athari kubwa zilizotokana na janga la COVID-19 amesema “Uchumi unaojali mazingira unahitajika ili kuhifadhi na kulinda mazingira yetu. Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi ynatoa muongozo kwa dunia kuhamia katika maendeleo yanayozingatia mazingira na kiwango cha chini ya hewa ukaa.” 

Uwekezaji zaidi wahitajika 

Akitoa wito wan chi zote kutimiza makubaliano ya mkataba wa kihistoria wa Paris Rais Xi amesema China itaongeza mchango wake wa kitaifa kwa kupotisha hatua na sera mpya. 

“Tunalenga kufikia ukomo wa hewa ukaa kabla ya mwaka 2030 na kutimiza lengo la kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2060. Tunatoa wito kwa nchi zote kusaka na kuratibu maendeleo ambayo yanazingatia mazingira ya yaliyo wazi kwa wote.” 

Amesema ushirikiano wa kimataifa wakayti Umoja wa Mataifa ukiwa ndio kitovu ni muhimu sana, na hivyo ametoa wito kwa nchi zote zilizoendelea kiuchumi kufanya yaliyo bora zaidi kwa maslahi ya umma, kuwajibika na kukidhi matarajio ya watu. 

Ahadi kwa China na kwa dunia 

Rais huyo wa Uchina amesema taifa lake limefanya juhudi kubwa kudhibiti virusi vya corona na kurejesha kwa haraka maisha ya kawaida na ukuaji wa uchumi, akiongeza kwamba ana imani kwamba wataweza kutimiza lengo la kutokomeza umaskini lililowekwa na malengo ya maendeleo endelevu muongo mmoja kabla ya ukomo wa malengo hayo. 

Ameongeza kuwa China itaendelea kufanya kazi kama mjenzi wa amani ya dunia, mchangiaji wa maendeleo ya kimataifa na mtetezi wa utulivu wa kimataifa. 

Ameyasema hayo wakati akitangaza kuingiza dola zingine milioni 50 kwenye mfuko wa Umoja wa Mataifa wa mpango wa msaada wa kupambana na COVID-19. 

Pia ameahidi dola milioni 50 za mfuko wa China na ushirika wa Kusini Kusini wa FAO awamu ya III, ametangaza kuongeza muda wa mfuko wa amani na maendeleo baina ya Umoja wa Mataifa na China kwa miaka mitano zaidi utakaoenda zaidi ya mwaka 2025. 

Zaidi ya hayo ametangaza kuanzisha kituo cha kimataifa cha Umoja wa Mataifa kuhusu elimu ya masuala ya anga na ubunifu na kituo cha kimataifa cha utafiti wa takwimu kubwa kwa ajili ya SDGs kusaidia kusongesha mbele ajenda ya maendeleo ya 2030. 

 

TAGS: China, COVID-19, SDGs , UNGA75 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter