Waokota takataka wanaweza kuwa washirika muhimu wa mazingira-UNICEF

9 Septemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kushirikiana na kampuni ya Conceptos Plasticos ya Columbia wanaendesha mradi wa kubadili takataka za plastiki kuwa matofali ya kujengea shule nchini Côte d’Ivoire. 

Pamoja na kuwa madhara ya plastiki yanafahamika, utafiti unaonesha kuwa katika miaka 30 ijayo, ulimwengu unaweza kuzalisha plastiki mara nne zaidi ya ambazo zimezalishwa hapo awali. 

UNICEF inaeleza kuwa kutafuta namna mbadala na bunifu za matumizi mbadala ya plastiki itakuwa muhimu kwa afya ya umma.  

“Bila kuwa na udhibiti wa taka za plastiki, uchafuzi wa maji ya chini ya ardhi unaweza kuziacha jamii nyingi bila maji salama. Mitaro iliyozibwa na plastiki inaweza kuendelea kusababisha mafuriko na kuharibu miundombinu. Na uchafuzi wa hewa kutokana na kuchoma majalala kunaweza kuleta hatari kubwa kwa mazingira na afya.” Inasema UNICEF.  

Yvonne Koffi ni mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda cha Conceptos Plasticos anaeleza namna wanavyofanya kazi akisema, “hapa niliposimama, ndipo tunapochukua taka za plastiki kuzibadili kuwa matofali ya plastiki. Hebu nikuoneshe inavyokuwa.”   

Msichana huyu pamoja na wenzake wanaonekana wakiwa wamevaa kofia ngumu, miwani na wengine wamejifunika midomo kwa barakoa.  

“Kwanza tunazichambua taka za plastiki na na kuziweka kwenye mashine ya kuzipondaponda. Kisha tunazibeba plasitiki zilizopondwapondwa kuzipeleka katika mashine nyingine ya kuziponda tena. Mashine inayofuata inatengeneza taka hizi kuwa kama tope zito na kulichanganya kisha tunakata katika vipandevipande vidogo. Mwishowe, tunaingiza lile tope zito la plastiki katika mtambo na matofali yanatoka nje.”  Anafafanua Yvonne. 

Kutokana na ufanisi wa wa gharama, uimara, na urahisi wa kuyapanga wakati wa ujenzi, matofali yaliyotengenezwa kutokana na taka za plastiki kwa asilimia mia moja yana uwezo wa kuvuruga muundo wa kawaida wa ujenzi na kuchochea soko la plastiki iliyorejelezwa kote ulimwenguni kama anavosema Yvonne kuwa, “kwa kutumia matofali hayo, tunajenga shule ili watoto waweze kwenda shule.”  

UNICEF inasema, “mamilioni ya wafanyakazi wa kukusanya taka katika majalala na mitaa ya miji kote duniani wanaweza kuwa washirika muhimu wa kudhibiti taka, kuinuliwa kutoka katika umaskini huku wakisaidia kuisafisha sayari yet una kutoa matofali kwa ajili ya mstakabali wa watoto wetu.”  

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud