Mkataba kupinga ajira kwa watoto waweka historia kuridhiwa na nchi zote wanachama:ILO

4 Agosti 2020

Nchi zote wanachama wa shirika la kazi duniani ILO wameridhia mkataba wa kupiga mifumo mibaya zaidi ya ajira kwa watoto duniani, mkataba namba 182 uliopitishwa mwaka 19999 limesema leo shirika hilo. 

Kwa mujibu wa ILO mkataba huo umekamilisha malengo ya kurdhiwa na wanachama wote baada ya mwanachama wa mwisho ufalme wa Tonga  kuuridhia mkataba huo ilipowasilisha rasmi sahihi yake kwa mkurugenzi mkuu wa ILO Guy Ryder leo Agosti 4 mwaka 2020. 

Shirika hilo limeongeza kuwa huu ndio mkataba uliodhiriwa haraka zaidi na wanachama wote katika historia ya shirika hilo tangu ulipopitishwa rasmi miaka 21 iliyopita kwenye mkutano wa kimataifa wa ILO. 

Kufuatia hatua hii mkurugenzi mkuu wa ILo Guy Ryder amesema “Kuridhiwa na nchi zote wanachama mkataba namba 182 ni jambo la historia , kwanza likimaanisha kwamba watoto wote sasa wana haki ya kisheria ya kulindwa dhidi ya mifumo mibaya zaidi ya ajira za watoto. Hii inadhihirisha mshikamano na ahadi ya kimataifa kwamba mifumo yote mibaya zaidi ya ajira za watoto kama vile utumwa, unyanyasaji wa kingono, matumizi ya watoto kwenye vita vya silaha au katika kazi zingine ngumu na za hatari ambazo zinaathiri afya ya watoto, ustawi wao wa kijamii na kiakili haina nafasi katika jamii yetu.” 

Akikaribisha hatua hiyo pia Katibu mkuu wa shirikisho la kimataifa la muungano wa biashara (ITUC) Sharan Burrow amesema “Kuridhiwa na nchi zote wanachama kwa mkataba huo namba 182 ni kumbusho la wakati muafaka la umuhimu wa viwango vya ILO na haja ya suluhu za pamoja za matatizo ya kimataifa. Ajira kwa watoto ni ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi na ni wajibu wa mikataba ya ILO na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kwamba mkataba huu unatekelezwa kikamilifu ikiwemo kupitia hatua katika mnyororo wa kimataifa.” 

Ameongeza kuwa kuridhiwa na wanachama wote kwa mkataba huo ni hatua nzuri ya kuelekea kutimiza ndoto za mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Kailash Satyarthi ambaye alisema “Ninaota kuwa na dunia ambayo imejaa watoto walio salama na usalama wa watoto, ninaota kuwa na dunia ambayo kila mtoto anafurahia uhuru wa kuwa mtoto.” 

ILO inakadiria kwamba kuna watoto milioni 152 walio katika ajira ya watoto kote duniani, milioni 73 kati yao katika kazi ambazo ni za hatari.  Na asilimia 70 ya ajira ya watoto inafanyika katika sekta ya kilimo na inahusiana kwa kiasi kikubwa na umasikini na ugumu wa wazazi kupata ajira zenye hadhi. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud