TANZBATT 7 yapatia msaada watoto yatima Kivu Kaskazini

13 Julai 2020

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC , watoto yatima wa kituo cha New Chance jimboni Kivu Kaskazini, wameshukuru msaada wa hali na mali kutoka kwa walinda amani wa Tanzania. 

Walinda amani kutoka Tanzania, kundi la 7, TANZBATT 7, wanaoongozwa na kamanda wa kikosi Luteni Kanali John Magnus Ndunguru, wanaohudumu katika kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC MONUSCO, jimboni Kivu Kaskazini  wanawasili kwenye kituo hiki cha yatima na kutoa misaada yao.

Koplo Nuru Hamis Mohammed ni miongoni mwa walinda amani walioshiriki kutoa misaada hiyo ambayo ni pamoja na sabuni za kufulia, vyombo vya jikoni, vinywaji na viatu.

Kwa upande wake, Jean-Claude Matondo ambaye ni mkurugenzi wa kituo hiki cha New Chance ameshukuru akisema kuwa, “tuna furaha kubwa sana kituo cha yatima cha New Chance, mara nyingi ndugu zetu watanzania wanatutembelea. Kwa mara nyingine natoa shukrani kwa dada yetu na pia rafiki kwa kazi nzuri anaendelea kufanya kwa kusaidia yatima. Hata kama ni kitu kidogo kwa Mungu ni kitu kabambe. Na huyu ambaye amesaidia na kitu kidogo, wakati akipata vitu vingi, anaweza kusaidia. Tunashukuru sana kwa kuendelea kusaidia hawa watoto yatima wa Congo.”

TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakikabidhi vifaa vya shule kwa Chifu wa kata ya Matembo iliyo mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Beni, nchini DRC.

Busu Lipasu ni Chifu wa eneo la Bambiro jimboni Kivu Kaskazini naye alikuwa shuhuda wa kupokea misaada hiyo ya watoto na anasema kuwa, “ninashukuru tena mara nyingine kwa kuweza kukumbuka watoto yatima wa Bambiro ambao ndugu yetu Cisse Jean-Claude Matondo anaendelea kuwalea na hana msaada wowote wa kuwagharamia. Lakini kutokana na ndugu zetu watanzania ambao wamewakumbuka kwa mara nyingine tena, ninasema Mungu awabariki, na mzidi sana kuwakumbuka na msiseme leo ndio mwisho, mje tena na tukutane hapa. Kwa niaba ya wakazi wote wa Bambiro nasema asante sana na tunasema watanzania Mungu awabariki.”

Kituo hiki cha New Chance, kina jumla ya watoto 73 ambao huchukuliwa tangu wakiwa na umri wa mwaka mmoja hadi wanapofika elimu ya juu. Solanji ni miongoni mwa watoto yatima waliolelewa na kituo hiki tangu akiwa na umri wa miaka mitatu na sasa yupo kidato cha tano na anasema, “tunashukuru sana kwa kuwa mko wazazi wema. Kwa kile ambacho mmetufanyia leo isiwe mara ya kwanza, zaidi muwe mnatumbuka na Mungu awatawalipa.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud