Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante TANZBATT_7 kwa mafunzo ya TEHAMA, sasa tunajiamini- Mkazi Beni 

Takriban nusu ya watu duniani kote wanatumia TEHAMA ikiwa ni asilimia 51.2 ya watu duniani ifikapo mwisho huu wa 2018
ITU
Takriban nusu ya watu duniani kote wanatumia TEHAMA ikiwa ni asilimia 51.2 ya watu duniani ifikapo mwisho huu wa 2018

Asante TANZBATT_7 kwa mafunzo ya TEHAMA, sasa tunajiamini- Mkazi Beni 

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wamechukua jukumu la kufundisha wakazi wa jimboni Kivu Kaskazini teknolojia ya mawasiliano kama njia mojawapo ya kuwajengea uwezo sambamba na ulinzi wa raia. 

Pamoja na majukumu mbalimbali ya ulinzi wa amani kwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, yanayofanywa na vikosi vya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa, katika kikosi chake cha kujibu mashambulizi, FIB kwenye ujumbe wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, kikosi cha 7, TANBZATT-7 kutoka Tanzania, kinachohudumu nchini humo, kimefanikiwa kuendesha mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, TEHAMA, kwa mafunzo ya kompyuta kwa raia. 

Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo ili kuendana sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia, yamechukua kipindi cha miezi minne na yanakamilika Januari mwaka 2021. 

Kapteni Renatus Kanyika ni afisa TEHAMA jwa TANZBATT 7 nchini DRC na anasema,”jukumu langu katika kikosi hiki ni kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano hasa inayotumia kompyuta pamoja na mawasiliano ya kawaida, yanaenda vyema kwa kadri yalivyopangwa. Lakini zaidi ya hayo, kama jukumu letu kuu la msingi la ulinzi wa amani katika DR Congo, pia huwa tunawasaidia wananchi wa DRC stadi mbalimbali ambazo tunazo.  Kwa hiyo kwa kushirkiana na ofisi ya mahusiano, tuliona ni vyema tukatoa elimu ya kompyuta kwa vijana wa DRC. Kwa hiyo tukaanzisha programu maalum ya kujifunza somo la kompyuta ambalo litalenga katika kuwapatia taaluma vijana hawa wa Congo, jinsi teknolojia ilivyo muhimu katika maisha yao kila siku.” 

Mkufunzi huyo mbobezi katika TEHAMA anazungumzia mapokeo na matarajio ya vijana na kile ambacho wanaacha kama alama na ukumbusho muhimu kwa jamii hiyo akisema, “lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo vijana hawa ili wafahamu umuhimu wa TEHAMA na hasa matumizi ya kompyuta katika maisha yao ya kila siku. Kwa mfano Umoja wa Mataifa mbali na shughuli zake za ulinzi wa amani, yapo makundi yanayofanya tafiti kuhusu ulinzi wa amani na huhitaji vijana kutoka hapa DRC kwa ajili ya kuwasaidia  ukusanyaji wa taarifa na kuziingiza katika kompyuta."

Soundcloud

Mkufunzi huyo amesema wanapowajengea uwezo kupitia mafunzo hayo, washiriki wanaweza kupata ajira na kulipwa ujira kwa kuwa wana uwezo wa kutumia kompyuta akisema kuwa," Umoja wa Mataifa inaendesha, na hata tafiti mbalimbali ambazo vijana wanaosaidia katika ukusanyaji wa data au taarifa mbalimbali wanawachukua kutoka DRC. Kwa hiyo mafunzo haya yamekuwa yana mafanikio na wengi wameonesha hamu kubwa ya kujifunza kwa bidii, na mimi kama kiongozi wa mafunzo na wakufunzi wenzangu, tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuwajengea uwezo wa kujifunza kwa bidii kwa kadri inavyokuwa ili waweze kupata nafasi ya kufahamu nafasi ya teknolojia katika maisha yao, lakini zaidi sana nafasi ya kufahamu kompyta katika matumizi mbalimbali kwenye maisha yao ya kila siku.” 

Kavuu Natalie ni  miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo na anasema, “tumefurahishwa sana na mafunzo haya, yatatunufaisha katika maisha yetu, hata ikiwa nyumbani, au kazini tumefurahi sana watanzania kutuwekea mafunzo haya, tunahakikisha kwamba tumejua kabisa kompyuta ili tukipata kazi haya ya kompyuta hatutashindwa kabisa. Tunashukuru sana watanzania na nasihi wanawake wenzangu ambao hawajafanya mpango wa kujifunza, waje kwani sisi tumejua kabisa na sasa ni wataalamu sasa, ni shule nzuri sana. Kwa sababu nilikuja sijui hata kitu kimoja lakini sasa nimejua kutumia kompyuta. Walimu nawashukuru sana na nawaaambia watanzania asante sana kwa kutufundisha kompyuta. “ 

Joshua Kapisa naye mnufaika anasema, “nilikuwa na hamu kubwa sana kujifunza kompyuta kwani itatusaidia kufanya kazi mbalimbali.  Kama mimi hapa ni mwalimu! Najua nikimaliza mafunzo nitakuwa tayari kuwafundisha wanafunzi wengine vizuri sana. Na nitaendelea kufanya kazi zangu bila shida. Haya mafunzo tuliomba kwa kuwa wale vijana wakitoka hapa watakuwa wamepata faida na wataweza kujitegemea kwenye maisha yao. Akifanya kazi ya mtu analipwa fedha. Haya masomo yana faida sana. “ 

Mafunzo haya yanakamilika siku chache zijazo ambapo kamanda wa kikosi cha TANZBATT_7 Luteni Kanali John Magnus Ndunguru atawakabidhi vyeti washiriki wa mafunzo.