Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa MINUSCA mjini Bangui waleta maridhiano baina ya waislamu na wakristo

Wakazi wa moja ya maeneo ya manispaa ya 3 ya mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Bangui wakifurahi wakati wakichota maji kutoka kisima kilichojengwa na MINUSCA kupitia miradi yake ya matokeo ya haraka, QIP.
MINUSCA/Hervé Serefio
Wakazi wa moja ya maeneo ya manispaa ya 3 ya mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Bangui wakifurahi wakati wakichota maji kutoka kisima kilichojengwa na MINUSCA kupitia miradi yake ya matokeo ya haraka, QIP.

Mradi wa MINUSCA mjini Bangui waleta maridhiano baina ya waislamu na wakristo

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSCA umetekeleza mradi wa maji na kusaidia kuleta utangamano baina ya jamii kwenye manispaa moja ya mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.

MINUSCA imejenga visima vitatu vya maji kwenye manispaa ya 3 ya maeneo ya  Sara, Yakite na Castors na kukidhi mahitaji ya wakazi wa eneo hilo waliokuwa wanakumbwa na uhaba mkubwa wa maji.

Uchimbaji wa visima hivyo ni kupitia miradi ya matokeo ya haraka, au QIP inayotekelezwa na MINUSCA ambapo Adam Roufai ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa ya 3 anasema wanashukuru sana mwa mradi huo wa maji kwa kuwa utasaidia katika usalama wa kiafya hususan wakati huu wa janga la virusi vya Corona au COVID-19“Maji ni muhimu sana kwa jamii hii ambayo imekosa kila kitu,” amesema Bwana Roufai.

Manispaa ya 3 kwa muda mrefu imekuwa kitovu cha ghasia baina ya makabila

Luteni Kanali Leila Zemzoumi ni afisa kutoka MINUSCA na anasema kuwa, “MINUSCA imejenga visima hivyo vitatu katika eneo la Sara-Yakite-Castors kwa sababu kulikuwepo na mizozo kupindukia ndani ya jamii na baina ya jamii. Na ukosefu wa maji ulichochea zaidi mapigano hayo baina ya jamii za waislamu na za wakristu. “

Kutekelezwa kwa mradi huu uliogharimu takribani dola elfu 46, kunafuatia kutiwa saini kwa mkataba wa ujirani mwema tarehe 23 mwezi Machi mwaka jana wa 2019 baina ya wakazi wa maeneo ya Sara, Yakite na Castors na  kila kisima kilijengwa kwenye eneo ambalo jamii ziliridhia.

Mchungaji Justin Nicolas Mbassi ni Katibu Mkuu wa mkataba wa ujirani mwema na anasema kuwa, “kimbunga kilisukuma upepo na umoja ambao walikuwa nao wazazi wetu ulitoweka. Lakini haya maji yamekuja kutuweka pamoja,  kutuunganisha na yamekuja wakati muafaka tulioazimia wa kuwa tena watu wamoja, taifa moja na kwa manispaa yetu kwani itatuunganisha wote.”

Visima vimenusuru wanawake, sasa jukumu la kulinda ni la vijana

 Visima vitatu vya maji ni nyongeza ya mgao wa maji safi yanayosambazwa na MINUSCA kwa gari Jeanne Kodona, Chifu wa eneo la Souma Potopoto anatoa shukrani kwa MINUSCA akisema kuwa, “kama kusingalikuwepo na haya maji, tusingaliweza kuishi kama tutakiwavyo. Tunashukuru MINUSCA ambayo imetujengea visima hivyo vya maji.

Uwepo wa visima hivi umeokoa wanawake ambao walikuwa wanatembea mwendo mrefu kufuata maji na Hawa Azoumi, mkazi wa Yakite ni shuhuda akisema kuwa, “tunashukuru sana walioanzisha wazo la kuchimba visima hivyo vya maji, awali tulikwenda mbali kusaka maji, lakini sasa maji yako karibu na yana ubora wa hali ya juu. Tunawashukuru sana.”

Jukumu la jamii hii sasa ni ulinzi wa vituo hivyo vya maji lakini Nicolas Tehun Pay Pay mkazi wa Yakite anawageukia vijana akisema kuwa, “Mimi sasa nina umri wa miaka 61, nadhani itakuwa vyema kwa vijana wa leo walinde  vyema mradi huu kwa sababu ni kwa ajili yao. Sifahamu, mimi pengine kesho au keshokutwa nitaondoka.”