Dunia iko katika janga la tsunami ya COVID-19: Guterres 

Hali baada ya tsunami ya mwaka 2018 kupiga ufukwe wa Palu, Indonesia.
UNICEF/Watson
Hali baada ya tsunami ya mwaka 2018 kupiga ufukwe wa Palu, Indonesia.

Dunia iko katika janga la tsunami ya COVID-19: Guterres 

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni siku ya uelimishaji kuhusu tsunami duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka dunia kuiba uzoefu wa maandalizi ya majanga kwenye hatua zilizopigwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na tsunami.

Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa siku hii amesema watu hivi sasa wanaishi katika dunia iliyoghubikwa na hatari ya majanga mengi na yaliyojipenyeza katika maendeleo ya binadamu. 

Ameongeza kuwa “Kwa sasa tunahaha kwa kile wengi wanachokielezea kama ni tsunami ya vifo na magonjwa kwa sababu ya COVID-19. Na usemi huu unakuja kirahisi kwa sababu ya kumbukumbu iliyosalia ya janga kubwa la kihistoria la tsunami la mwaka 2004 kwenye bahari ya Hindi ambalo lilikatili maisha ya watu zaidi ya 227,000”. 

Kwa mantiki hiyo Guterres amesema maandalizi ya magonjwa ya milipuko kama hili la COVID-19 yanaweza kuiga uzoefu mkubwa kutoka kwa hatua zilizopigwa katika kupunguza kiwango cha kupotea kwa maisha ya watu kutokana na janga la tsunami. 

Ameweka bayana kuwa hivi sasa kuna mifumo bora ya kutoa taharadhari ya mapema wakati maeneo ya pwani yanapokuwa hatarini na Umoja wa Mataifa unashirikiana na wadau kote duniani kuelimisha umma, kufanya majaribio ya dharura, kuandaa njia za uokozi na kuhamisha watu na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha vifo vya watu wengi vinaepukwa endapo litakatokea janga lingine la tsunami. 

Naye mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu upunguzaji wa hatari ya majanga (UNDRR)Mami Mizutori katika ujumbe wake amesema COVID-19 ni kumbusho la umuhimu wa maandalizi ya majanga ,“COVID-19 imetufunza kwamba kujiandaa na kuwa tayari kunaokoa maisha na ajira. Majanga hayasubiri zamu yao , nchi nyingi ambazo sasa zinakabiliwa na COVID-19 pia zina majanga mengine kama typhoon, vimbunga na matetemeko ya ardhi, hivyo hatuwezi kupumzika.” 

 Amesisitiza kuwa nchi za Asia, Amerika Kusini na Caribbea zimejifunza kutokana na tsunami na sasa zimejijengea utamaduni wa kuelimisha umma, kuchukua tahadhari na kubwa zaidi kujiandaa. 

Maudhui ya siku ya mwaka huu ni “kuimarisha udhibiti wa hatari za majanga” na siku ya uelimishaji kuhusu tsunami duniani kuadhimishwa kila mwaka Novemba 5.