Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Mradi wa wakimbizi kutengeza sabuni  Za'atari unafanyika wakati muafaka:UNHCR

Watoto wa shule ya msingi nchini Jordan wakinawa mikono
©UNICEF/Jordi Matas
Watoto wa shule ya msingi nchini Jordan wakinawa mikono

 Mradi wa wakimbizi kutengeza sabuni  Za'atari unafanyika wakati muafaka:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kwa kutumia bidhaa za asili, wanawake wakimbizi kwenye kambi kubwa zaidi nchini Jordan wanatengeneza sabuni na kugawa kwa familia zilizo na mahitaji kwa ajili ya kusaidia katika kuzuia kuenea kwa virusi vya corona au COVID-19

Katika kambi ya wakimbizi ya  Za’atari tunakutana na wanawake wakiwa katika shughuli ya kutengeneza sabuni, kupitia video ya shirika la Umoja wa Msataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, hapa wanaonekana wakikatakata glycerin moja ya kiungo katika sabuni zao.

Wanawake hawa walipokea mafunzo kutoka Shirika la , UNHCR kama sehemu ya mradi wa Za’atari unaolenga kutoa mafunzo kwa wanawake. Um Mustafa, ni meneja, wa kikuundi cha Made in Za’atari ikimaanisha ilichotengenezwa Za’atari,“Sisi ni kundi la wanawake waliojifunza kuengeneza sabuni kwa ajili ya kusaidia familia zetu na sisi wenyewe.”

Wanawake hawa wanatumia viungo vya asili lakini pia kuna viungo vya ziada, kwenye video hii ya UNHCR wanaonekana wakimimina mchanganyiko wa rangi tofauti kwenye vyombo vya plastiki vyenye maumbo tofauti,“Tunaongeza pia viungo tofauti kwa mfano rangi, marashi na na kileo kwa ajili ya kuifanya iwe bidhaa sio tu inayosafisha lakini pia inayotakasa mikono.”

Kwa upande wake Irene Omondi, meneja wa kambi hiyo ya Za’atari anasema,“Ni mfano mzuri wa kutoa kwa jamii na kuzingatia usafi wakati kama huu kama UNHCR tunawajengea uwezo wanawake hawa na kuwapa mafunzo ya mradi wa Made in Za’atari kwa ajili ya kutengeneza vitu tofauti na kutumia stadi zao kutengeneza sabuni. Wanafanya kazi nzuri.”

Lengo la kutengeneza sabuni hizo ni lipi? Um anasema,“Tunatengeneza sabuni kwa ajili ya kusaidia wakimbizi wa Syria kwa sababu ni bidhaa muhimu.”

Programu hii sio tu inasaidia wanawake kuimarisha stadi zao lakini inahakikisha kwamba wakimbizi wanawaeza kunawa mikono yao kwa njia salama.