Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani Tanzania inaonesha kuendelea kutetereka kwa uhuru wa raia-UN

Wananchi katika moja ya mitaa ya jiji la Dar es salaam, Tanzania. Picha ya MAKTABA
UN-Habitat/Julius Mwelu
Wananchi katika moja ya mitaa ya jiji la Dar es salaam, Tanzania. Picha ya MAKTABA

Hukumu dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani Tanzania inaonesha kuendelea kutetereka kwa uhuru wa raia-UN

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR kupitia taarifa yake iliyoitoa hii leo jumanne Machi, 17, 2020 mjini Geneva Uswisi na Addis Ababa Ethiopia imeeleza kuwa hukumu ya hivi karibuni dhidi ya viongozi wa kisiasa nchini Tanzania ni ushahidi tosha wa kutetereka kwa uhuru wa raia nchini humo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hukumu ya hivi karibuni ya viongozi nane wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA pamoja na kiongozi mmoja aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, kwa makosa ya uchochezi na mkusanyiko usio halali ni ushahidi mwingine wa kutatiza wa kutesa uhuru wa umma nchini humo. 

Hukumu ilitolewa na mahakama mjini Dar es Salaam tarehe 10 ya mwezi huu wa Machi ambapo watuhumiwa 9 walikutwa na hatia katika makosa 12 kati ya makosa 13 yaliyohusiana na maandamano yaliyofanyika mnamo mwezi Februari 2018 ambayo waliyaandaa na kushiriki. Walikuwa wamepanga na kushiriki katika mikutano ya hadhara katika mji mkuu kati ya tarehe 1 na 16 Februari 2018. Wakati wa moja ya maandamano, mwanafunzi wa umri wa miaka 21 alipigwa risasi na kuuawa wakati maafisa wa polisi walijaribu kuwazuia waandamanaji. Kumekuwa hakuna uchunguzi hadi leo juu ya kifo hiki na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa haijui jaribio lolote la kushikilia mtu yeyote ambaye atawajibika. 

Viongozi Freeman Mbowe, Peter Msigwa, Salum Mwalimu, John Mnyika, Esther Matiko na Vincent Mashinji aliyeihama CHADEMA walishitakiwa mnamo mwezi Machi mwaka 2018. Halima Mdee, John Wegesa na Esther Bulaya wao walishitakiwa tarehe 13 Aprili mwaka huo huo wa 2018. Watuhumiwa hao walihukumiwa na kutakiwa kulipa faini ya jumla ya shilingi za kitanzania milioni 350 ambazo ni takribani sawa na dola za kimarekani 152,000 au vinginevyo watumikie kifungo cha miezi mitano jela.

Taarifa imeeleza kuwa kutokana na viongozi hao kushindwa kulipa faini kwa haraka siku hiyo ya Machi 10, viongozi hao tisa walipelekwa katika gereza la Segerea lililoko mjini Dar es Salaam. Hata hivyo kupitia katika kampeni iliyoendeshwa na CHADEMA kupitia mitandao ya kijamii, ilifanikiwa kuchangisha kiasi cha fedha kilichokuwa kinatakiwa kulipwa na hivyo viongozi waliokuwa wanashikiliwa wakaachiwa.

Ripoti zilizopokelewa na Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mnamo tarehe 13 Machi kulikuwa na vurugu nje ya gereza wakati Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alipokuwa akiachiwa, ambapo askari polisi na walinzi wa gereza walitumia mabomu ya machozi na virungu kuwatawanya watu. 

“Takribani viongozi 25 wa CHADEMA na wanachama wanaripotiwa kukamatwa na kisha kuachiwa kwa dhamana ya polisi.” Imeeleza sehemu ya taarifa ya Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Aidha taarifa hiyo imesema kuwa hukumu ya hivi karibuni inaonesha kile kinachoonekana kuwa ni mkakati unaoendelea wa serikali kutumia mfumo wa kijinai kuwalenga wakosoaji wake, kuweka faini kubwa au vifungo vya gerezani kwa wapinzani, wanahabari na viongozi wa asasi za kiraia. Baadhi ya watu, wakiwemo baadhi ya wanachama wa CHADEMA, wamekabiliwa na mashitaka na kuitwa mahakamani mara kwa mara. 

Mnamo mwezi Juni mwaka 2016, Rais John Magufuli wa Tanzania alitangaza zuio la shughuli za kisiasa hadi mwaka huu wa 2020, zuio ambalo bado linaendelea ijapokuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo umepangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. 

“Nafasi ya demokrasia na ya kiraia imepungua, karibia sawa na bure nchini Tanzania.Kupigwa marufuku maandamano ya kisiasa kwa ujumla ni kizuizi kisicho na usawa juu ya haki ya kukusanyika kwa amani na inaweza kuwa ya kibaguzi. Serikali inapaswa kuiondoa mara moja marufuku hii, na kufuata majukumu yake ya kimataifa ya kuheshimu haki za binadamu, pamoja na haki ya uhuru wa mkutano na amani, na uhuru wa kujieleza.”  Imesisitiza taarifa hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.