Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

China inawajibika kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mkoa wa Xinjiang: ripoti ya OHCHR

Kamishna Mkuu Michelle Bachelet wakati wa ziara yake nchini China, huko Ürümqi, Xinjiang Uyghur China.
OHCHR
Kamishna Mkuu Michelle Bachelet wakati wa ziara yake nchini China, huko Ürümqi, Xinjiang Uyghur China.

China inawajibika kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mkoa wa Xinjiang: ripoti ya OHCHR

Haki za binadamu

Ripoti iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya ofisi ya kamishna mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) kuhusu kile China inachokiita eneo linalojiendesha la Xinjiang Uyghur (XUAR) imehitimisha kuwa na "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya Uyghur na wengine ambao wengi wao ni jumuiya za Waislamu.”

Ripoti hiyo iliyochapishwa leo Jumatano kufuatia ziara ya kamishna mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet mwezi Mei, inasema kwamba "madai ya mifumo ya mateso, au unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na matibabu ya kulazimishwa na hali mbaya ya kizuizini, ni ya kuaminika, kama vile madai ya matukio ya watu binafsi ya unyanyasaji wa kingono na kijinsia."

Katika tathmini yenye maneno makali mwishoni mwa ripoti hiyo, OHCHR inasema kwamba kiwango cha kuwekwa kizuizini kiholela dhidi ya watu wa Uyghur na watu wengine, katika muktadha wa "vizuizi na kunyimwa haki za msingi zaidi, zinazofurahiwa binafsi na kwa pamoja, kunaweza kujumuisha uhalifu wa kimataifa, na hususan uhalifu dhidi ya binadamu.”

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
UN Photo/Antoine Tardy
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet


Uhakiki mkali

Ofisi ya haki za Umoja wa Mataifa imesema kwamba ripoti ya leo Imetokana na tathmini ya kina ya nyaraka za maandishi ambazo sasa zinazopatikana kwenye ofisi hiyo, na uhakiki wake wake umetathminiwa kwa mujibu wa viwango vya mbinu za kawaida za haki za binadamu.
“Uangalifu hasa ulitolewa kwa sheria, sera,takiwmu na taarifa za Serikali yenyewe. Ofisi pia iliomba habari na kushiriki katika mazungumzo na kubadilishana masuala ya kiufundi na China katika mchakato wote.” Imesema ripoti

Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye siku ya mwisho ya muhula wa Bi. Bachelet wa miaka minne madarakani, inasema ukiukaji huo umefanyika katika muktadha wa madai ya serikali ya China kwamba inawalenga magaidi miongoni mwa jamii ya wachache ya Uyghur kwa mkakati wa kukabiliana na itikadi kali unaohusisha matumizi ya kile kinachoitwa vituo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETCs), au kambi za kuelimisha upya.
OHCHR ilisema kuwa sera ya serikali katika miaka ya hivi karibuni huko Xinjiang "Imesababisha mifumo iliyoingiliana ya vikwazo vikali na visivyofaa kwa masuala mbalimbali ya haki za binadamu."

Hata kama mfumo wa VETC uko kama China inavyosema, "umepunguzwa wigo au kufungwa", imesema OHCHR, na kuongeza kuwa "sheria na sera zinazouunga mkono zinaendelea kuwepo, na kusababisha kuongezeka kwa matumizi ya kifungo.”
Mifumo ya kuwekwa watu kizuizini kiholela na mifumo inayohusiana ya unyanyasaji tangu 2017, imesema OHCHR, "Inakuja nyuma ya pazia kubwa la msingi wa ubaguzi dhidi ya Uyghur na watu wengine walio wachache.”

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu Michelle Bachelet akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva
© OHCHR/Anthony Headley
Kamishina Mkuu wa haki za binadamu Michelle Bachelet akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva

Ukiukaji wa sheria za kimataifa

"Hii imejumuisha vikwazo vya ukamataji wa kiholela na vya kibaguzi kwa haki za binadamu na uhuru wa msingi, kinyume na sheria na viwango vya kimataifa", ikiwa ni pamoja na vikwazo vya uhuru wa kidini na haki za faragha na kutembea.
Zaidi ya hayo, ripoti hiyo imesema kuwa sera za serikali ya China katika eneo hilo "zimevuka mipaka, kutenganisha familia, kukata mawasiliano, na kuweka mifumo ya vitisho dhidi ya jamii kubwa iliyotawanyika ughaibuni ya Uyghur ambayo imekuwa ikizungumza kuhusu hali ya nyumbani.”
OHCHR inasema kuwa serikali ya China "Inabeba jukumu la msingi la kuhakikisha kwamba sheria na sera zote zinatii sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuchunguza mara moja madai yoyote ya ukiukwaji wa haki za binadamu, kuhakikisha uwajibikaji kwa wahalifu, na kutoa haki kwa waathirika..”

Guterres asisitiza uhuru wa ofisi ya haki za binadamu

Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wa kawaida wa Mchana Katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani siku ya Alhamisi( 01 Septemba 2022)  Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, amesema Katibu Mkuu Antonio Guterres amesoma tathmini ya OHCHR, ambayo "inabainisha wazi ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo la Xinjiang nchini China."

Dujarric alisema Katibu Mkuu "anamatumaini makubwa kwamba Serikali ya China itachukua mapendekezo yaliyotolewa katika tathmini", huku akibainisha pia kwamba ripoti hiyo "pia inasisitiza umuhimu wa uhuru" wa OHCHR.

Akijibu swali kuhusu uhusiano huo utatoa nini katika siku zijazo, Dujarric alisema Katibu Mkuu "anathamini ushirikiano wa kimfumo kati ya China na Umoja wa Mataifa katika masuala mengi. China ni mshirika wetu wa thamani sana, na tunamatumaini makubwa kwamba ushirikiano utaendelea," na tukahimiza "ni muhimu kwa kila mtu kuona namna wachina watakakavyo itikia" kwa ripoti hiyo ya kina.