Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Afrika zizalishazo mafuta kupoteza dola bilioni 65 kutoka na virusi vya Corona 

Wahudumu wa afya nchini Misri katika harakati za kudhibiti virusi vya Corona kwenye uwanja wa ndege wa Luxor nchini Misri
Khaled Abdul Wahab
Wahudumu wa afya nchini Misri katika harakati za kudhibiti virusi vya Corona kwenye uwanja wa ndege wa Luxor nchini Misri

Nchi za Afrika zizalishazo mafuta kupoteza dola bilioni 65 kutoka na virusi vya Corona 

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya uchumi barani Afrika, UNECA, imeonya kuwa janga la virusi vya Corona lililokumba dunia hivi sasa litasababisha nchi za Afrika zinazozalisha mafuta kupoteza dola bilioni 65.

Katibu Mtendaji wa UNECA, Vera Songwe amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa, Ethiopia hii leo kuwa hali hiyo ni dhahiri kwa kuwa mapato kutokona na mafuta yatashuka kwa kuwa bei ya mafuta inaporomoka.

Halikadhalika amesema suala kwamba China ambayo ni mdau kubwa wa biashara Afrika amekumbwa na virusi vya Corona au COVID-19, nalo pia litaathiri biashara barani humo.

“Afrika inaweza kupoteza nusu ya pato lake la taifa kutoka asilimia 3.2 hadi asilimia 2 kutokana na sababu hizo za mafuta, virusi kukumba China na pia kuharibiwa kwa mnyonyoro wa usambazaji wa bidhaa,” amesema Bi.Songwe akitaja muunganiko wa usambazaji wa bidhaa baina ya bara la Afrika na Ulaya, China na Marekani.

Amesema janga la Corona linasababisha bara la Afrika kuingia gharama ambazo halikutarajia la dola bilioni 10.6 katika afya ili kuzuia virusi hivyo kuenea huku kupotea kwa mapato kunaweza kusababisha madeni yasiyolipika.

COVID-19 na mafuta

Akifafanua kuhusu mafuta, Bi. Songwe ametolea mfano wa Nigeria akisema kuwa “COVID-19 inaweza kupunguza mauzo ya nje ya Nigeria kwa mwaka 2020 kwa kati ya dola bilioni 14 na dola bilioni 19 na kwamba kwa Afrika, virusi hivyo vinaweza kusababisha mapato ya bara hilo yatokanayo na mauzo ya mafuta kwa  mwaka 2020 yapungue wa dola bilioni 101.”

COVID-19 kusababisha watu kupoteza ajira zao

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNECA akageukia pia utumaji wa fedha kutoka nje ya bara hilo pamoja na utalii akisema kuwa navyo vimeathiriwa na virusi vya Corona duniani kote na hivyo kusababisha pia kupungua kwa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, masoko ya ndani ya fedha kusinyaa na uwekezaji kusuasua na hivyo watu kupoteza ajira.

Dawa za binadamu nazo zinaweza kuongezeka bei

Kwa upande wa dawa nazo amesema zile zinazoagizwa kutoka Ulaya na maeneo mengine yaliyokumbwa na Corona zinaweza kupanda bei na  hata upatikanaji wake miongoni mwa waafrika ukapungua.

Uhakika wa chakula nao ni tatizo wakati huu wa Corona ambapo Bi. Songwe amesema, “wakati huu ambapo takribani theluthi mbili ya nchi za Afrika zinaagiza vyakula muhimu kutoka nje, uhaba wa chakula unatia hofu kubwa.”