Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 kuporomosha uchumi wa nchi za Afrika kusini mwa Sahara kwa asilimia 1.6- IMF

Waendesha teksi nchini Liberia wakati wa janga la Ebola mwaka 2014. Janga la COVID-19 nalo linatishia uchumi wa nchi zinazoendelea hususan za Afrika na dola bililoni 220 zinakadiriwa zitapotea.
UNDP/Morgana Wingard
Waendesha teksi nchini Liberia wakati wa janga la Ebola mwaka 2014. Janga la COVID-19 nalo linatishia uchumi wa nchi zinazoendelea hususan za Afrika na dola bililoni 220 zinakadiriwa zitapotea.

COVID-19 kuporomosha uchumi wa nchi za Afrika kusini mwa Sahara kwa asilimia 1.6- IMF

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la fedha duniani, IMF limetaja mambo matatu muhimu ya kuzingatiwa ili kuweza kupunguza madhara ya kibinadamu na kiuchumi yatokanayo na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
 

IMF imesema hayo ripoti yake ya leo iliyotolewa jijini Washington DC kuhusu mtazamo w shirika hilo kwa uchumi wa mataifa hayo wakati huu ambapo shirika hilo limesema janga la COVID-19 litasababisha uchumi wa mataifa hayo ya Afrika kitasinyaa kwa asilimia 1.6, kiwango cha juu zaidi cha mporomoko kuwahi kurekodiwa.

“Janga hili litafuta maendeleo ya hivi karibuni kwenye ukanda wote na hata kwa miaka ijayo,” amenukuliwa Abebe Aemro Selassie, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika IMF akisema kuwa viashiria vyote ni kwamba, “COVID-19 itakuwa na madhara makubwa ya kibinadamu na kiuchumi, uchumi wa dunia ukitwama, udhibiti wa fedha ukiongezeka, bei za bidhaa zinazouzwa nje zikiporomoka na kutibuka kwa shughuli za kiuchumi kutokana na hatua za kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona.”

Mathalani amesema vipato vya watu vimeporomoka na hivyo kuongeza pengo la ukosefu wa usawa, hatua za watu kutochangamana kuzuia watu wengi kushindwa kupata kipato chao.

Ni kwa mantiki hiyo mkuu huyo wa Idara ya Afrika ya IMF ametaja hatua muhimu tatu ambazo amesema ni muhimu ili kudhibiti gharama za kiuchumi zitokanazo na COVID-19.

Hatua ya kwanza ni kupatie kipaumbele ili kuongeza fungu la fedha kwenye sekta ya afya ya umma ili kudhibiti mlipuko bila kujali bajeti ya nchi. Pili ni kuhakikisha kuwa msaada mkubwa na unatolewa wakati muafaka akisema kuwa, “sera zinapaswa kujumuisha uhamishaji wa fedha au msaada wa vitu kwa kaya maskini wakiwemo wafanyakazi vibarua. Msaada pia ulenge sekta zilizodhurika zaidi. Uwezo wa nchi kupata fedha unategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kupata fungu la msaada kutoka jamii ya kimataifa.”

Ametaja hatua ya tatu kuwa ni será za fedha lazima ziwe na dhima muhimu katika kuendeleza kampuni na ajira.
Mkuu huyo wa Idara ya Afrika, IMF amesema kuwa katika kusaidia hatua za ndani, hatua zinazoratibiwa na wadau wote wa maendeleo ni muhimu.

Amesema IMF inashirikiana na wadau hao ambao ni Benki ya Dunia, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Benki ya Maendeleo Afrika na Muungano wa Afrika ili kukabili haraka janga la COVID-19.

Bwana Selassie amesema IMF imejiandaa kutoa dola bilioni 11 kwa nchi 32 za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambazo ziliomba msaada wiki za karibuni na tayari baadhi yao zimeshapata zikiwemo, Burkina Faso, Chad, Gabon, Ghana, Madagascar, Niger, Rwanda, Senegal, na Togo.

Amesema kuwa fedha hizo kwa nchi maskini zaidi na zilizo hatarini zaidi ni kutoka katika mfuko wa IMF wa kudhibiti majanga akisema wakati huu shirika hilo linahitajika zaidi na wanachama ili kuweza kupunguza mzigo wa gharama za kwenye sekta ya afya.